NA GODFREY NNKO
WANAWAKE watumishi wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) wameshiriki katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Dar es Salaam kimkoa yameadhimishwa katika Viwanja vya Leaders.
Maadhimisho hayo yameongozwa na Kaulimbiu inayosema "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji".
Aidha, katika kuadhimisha kilele cha siku hiyo,mgeni rasmi ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Limi Mihama ambaye ni Afisa Tawala Mwandamizi katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) amesema,shirika hilo linatambua mchango wa wanawake na ndiyo maana limewapa kipaumbele kufika katika maadhimisho haya muhimu duniani.
"Shirika linatambua mwanamke ndiyo msingi wa nyumba,na hata ukiangalia pia kauli mbiu ya shirika linatambua pia msingi wa nyumba kama mwanamke na ukizingatia Rais tuliye naye ni mwanamke kwa hiyo tunapata nguvu kuwa wanawake tunaweza, wanawake ni jeshi kubwa.
"Na sisi tunaungana na wanawake wote duniani kuadhimisha siku hii muhimu na adhimu kwa wanawake,shirika la nyumba tunalijenga taifa."
Pia, amewataka wanawake kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakiamini kuwa wanaweza.

"Tunao wanawake ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha miradi yetu ya NHC inakwenda mbele.
"Ukiangalia tunao mradi wa Samia Housing Scheme ambao upo Kawe, unaongozwa na Mhandisi mwanamke.
"Kwa hiyo, tunajivunia kwamba wanawake wanaweza na wakati mwingine kushinda hata wanaume, kwa hiyo wanawake tunaweza."

"Sisi kama Shirika la Nyumba la Taifa tunajivunia kwamba shirika letu kwa maana ya viongozi wetu kuanzia Mkurugenzi Mkuu hadi Bodi ya Wakurugenzi wameweza kuwapa kipaumbele wanawake."
Amesema, imani hiyo imeenda mpaka kwa baadhi ya kurugenzi na miradi inaendeshwa na kusimamiwa na wanawake ndani ya shirika hilo.
"Ukiachilia mbali kwa upande wa shirika, Siku ya Wanawake Duniani kitaifa mwaka huu ni ya kipekee sana, kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameipa kipaumbele sana na yeye ndiye mgeni rasmi kule jijini Arusha.
"Lakini, pia Mheshimiwa Rais ameweza kuchagua wanawake katika nyadhifa mbalimbali za kitaifa ikiwemo mawaziri na wakurugenzi wa taasisi.
"Lakini, pia Mheshimiwa Rais ameenda mbali zaidi ameweza kuwasaidia wanawake kupata mikopo ya asilimia 10 ambayo inawainua wanawake wa Tanzania na wanaweza kumudu na kuhudumia familia zao."
Pia, amesema jitihada za Rais Dkt.Samia zimewezesha wanawake kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua muhimu katika kulinda afya za wanawake na mazingira.
Katika hatua nyingine, Lilian Mushi amesema wao kama wanawake wa NHC wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha shirika linafanikisha makazi bora na nafuu kwa Watanzania.
"Ni nyumba ambazo kila Mtanzania anaweza akapanga au akanunua."