ZANZIBAR-Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kuanzia sasa watashirikiana kuiimarisha taaluma ya habari na utangazaji kwa kuinua vipaji vya watendaji wao kuwawezesha kufanya kazi katika viwango vinavyokubalika kisekta.
Hatua ilifikiwa kufuatia kuwepo kwa pengo katika tasnia hii ambapo matarajio ya vijana wanaoteuliwa kufanya kazi kwa vitendo hawakidhi vigezo vinavyotakiwa katika fani ya habari.
Makamu Mkuu wa SUZA Prof. Moh’d Makame Haji na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Bwana Bukini walifikia makubaliano hayo kufuatia mazungumzo yaliyofanyika ofisi za makao makuu ya Chuo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja tarehe (26/03/2025) yaliyowashirikisha wanataaluma na watendaji kutoka ZBC
Katika makubaliano hao viongozi hao walikubaliana kutengeneza vijana mahiri katika fani hii ili kuepusha wimbi la vijana waliokuwa tayari kufanya kazi kwa kujitolea mfumo ambao haukubaliki serikalini.
"Tangu tumefanya ‘reform’ ZBC miaka miwili iliyopita tumeona kuna pengo kati ya mahitaji ya soko kwenye na taaluma wanazokuja nazo kutoka vyuoni, tumetengeneza namna ya wanafunzi wengi zaidi kuja kupata uzoefu, bila shaka mpango huu utakuwa wazi mwaka mzima,’’alisema Bukini.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo Shirika lina mkakati wa mkakati wa kuwachukua vijana wengi zaidi kwenye mazoezi ya vitendo hali ambayo itachangia kuleta ufanisi wakati watakapokuwa tayari kuanza ajira rasmi.
"Umefikia wakati tutengeneze vijana wenye ujuzi, akisimama mtu akizungumzia suala fulani au akifanya mahojiano na mtu mwengine mtaalamu na yeye anapaswa kuwa na utaalamu wa jambo hilo badala ya kugusia gusia tu juu juu,’’alifahamisha.
Makamu Mkuu wa SUZA Prof. Moh’d alisema amefarajika kwa ZBC kutaka kushirikiana na SUZA katika sekta hii na kusema kuwa ana matarajio makubwa kupatikana ufanisi katika tasnia hii.
Alisema SUZA kinaendelea kuongeza wigo wa kuwa na programu mpya za masomo ambazo zitaanza kutumika rasmi mwezi Oktoba huku matarajio ya kuongeza wanafunzi wapya yanatarajiwa kufikia 1500 mwakani.
Aliongeza kuwa taasisi anayoiongoza inajikita kutekeleza sera, dira na mipango mikuu ya maendeleo ambapo inafanya tafiti na kuendelae kuzalisha wataalamu ambao ndio wanaotumika katika taasisi mbali mbali.
‘’Tuna ushirikiano na taasisi nyingi, wanachama wa Jumuia mbali mbali za ndani na nje ya nchi, ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati, Afrika kwa ujumla, Jumuia ya Madola na nyengine kadhaa’’, alieleza.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Haji ameagiza kuanza kutekelezwa mara moja kwa kuandaliwa hati ya makubaliano itakayowaongoza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Ushirikiano wa mashirika hayo mawili, unatarajiwa kuwajengea zaidi uwezo wanafunzi katika Skuli ya Habari na watendaji katika idara zake za habari za SUZA kwa kuwawezesha kufanya kazi zao kwa kujitegemea zaidi kama mtu mmoja kupiga picha na kuihariri, kuandika habari na kuhariri habari hiyo, mtangazaji na mzalishaji wa vipindi, na mtendaji ambaye atashughulia masuala ya Social media na kubadilishana wataalamu katika sekta hiyo kwa tasisi za habari za ZBC.
Tags
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)
Habari
Zanzibar Broadcasting Cooperation (ZBC)
Zanzibar News