Taarifa muhimu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma,makosa kadhaa yabainika kwa watumishi

DODOMA-Tume ya Utumishi wa Umma ilifanya Mkutano wake Na. 3 kwa Mwaka wa Fedha2024/2025 kuanzia tarehe 03/03/2025 hadi 21/03/2025 chini ya Mwenyekiti wake Jaji (Mst.) Hamisa H. Kalombola ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Tume za Utumishi wa Umma Afrika (AAPSCOMS), Kanda ya Afria Mashariki. 

Mkutano huo ulifanyika kwa mamlaka Tume iliyonayo chini ya Vifungu vya 10(1) na 25(1)(b) vya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (Marejeo ya Mwaka 2019).

Katika Mkutano huo, Tume ilitekeleza majukumu mbalimbali ambapo kuanzia tarehe 03/03/2025 hadi 06/03/2025, Tume ilifanya ziara ya kujifunza pamoja na kutoa elimu ya masuala ya Kiutumishi katika Taasisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali PaKazi (OSHA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) jijini Dar es Salaam.

Aidha,kuanzia tarehe 10/03/2025 hadi 21/03/2025, Tume ilipitia, kujadili na kuamua Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma yaliyowasilishwa mbele yake kwenye Ukumbi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika Jiji la Dodoma ambapo jumla ya Rufaa na Malalamiko 87 yaliwasilishwa na kutolewa uamuzi katika mchanganuo ufuatao:-

(i)Rufaa 62;na
(ii)Malalamiko 25.

Katika rufaa zilizowasilishwa na kuamuliwa, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi ni:-

(i) Kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma;

(ii) Utoro kazini;

(iii) Kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo;

(iv) Uzembe kwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo;na

(v) Wizi wa mali za Umma.Aidha,katika Mkutano huo, Warufani 24 na Warufaniwa 4 waliomba na kuruhusiwa kufika mbele ya Tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa walizoziwasilisha. 

Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi waUmma za mwaka 2022. Aidha, Tume ilipitia Taarifa mbalimbali za Utekelezaji wa Majukumu yake.

Tume inaendelea kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuendelea kuzingatia Sheria,Kanuni Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma ili kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, hali inayoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu au za kijinai. 

Ni muhimu pia kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma kuendelea kuzingatia Sheria wakati wa kushughulikia stahili, malalamiko na mashauri ya nidhamu ya Watumishi ili haki si tu itendeke,bali ionekane inatendeka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news