GEITA-Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe. William Lukuvi amesema Tanzania imebahatika kuongozwa na viongozi wanaojali utu na kutanguliza maslahi ya taifa mbele,hivyo tunamshukuru Mungu kwa kuwafanya sehemu ya historia kwa sababu taifa linaendelea kushuhudia mazuri waliyofanya kwa ajili ya nchi.
Waziri Lukuvi ametoa kauli hiyo tarehe 17 Machi, 2025 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada ya Misa Takatifu ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mt. Yohaba Maria Muzevi Chato.
“Leo tunadhimisha miaka Minne tangu tondokewe na mpendwa wetu Hayati Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hali ya kibinadamu si rahisi kusahau kumbukumbu ya kuondokewa na mpendwa wetu kwa jamii inayomfahamu na kujumuika naye katika maswala mbalimbali ya kitaifa”.
Aidha, amebainisha kuwa, Hayati Ally Hassani Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uhai wake aliwahi kusema, “maisha ya mwanadamu ni hadithi tuu, basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa wale watakaosimuliwa”, hii inamaanisha viongozi waliopita wameishi vyema na ndio maana tuna ujasiri wa kusimulia yaliyomema katika kumbukizi zao na kuendelea kusimulia yaliyofanywa na Hayati Dkt, John Pombe Magufuli.
“Hayati Dkt, John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi aliyejali watu na rasilimali za nchi yake na mchamungu hivyo tutaendelea kushirikiana na familia katika kumuenzi, kumuombea na kutangaza mema aliyoyafanya katika jamii na kama baba wa familia na kiongozi wa taifa letu,” alieleza.
Aidha, Waziri Lukuvi amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa karibu na familia tangu wakati wa uhai wa mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mpaka sasa.
“Upendo na ukaribu wake kwa familia umedhihirishwa kwa mambo mengi, mambo mengine tunayaona na yapo mengine familia wanayajua na sisi wengine hatuwezi kuyaona ndio maana katika matukio muhimu kama haya familia imekuwa ikimualika moja kwa moja, na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani amekuwa akiitikia mialiko hiyo kwa kushiriki yeye mwenyewe au kutuma miongoni mwa wasaidizi wake kuja kumuwakilisha pale anapokuwa na majukumu mengine ya kitaifa” alisema Waziri Lukuvi.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amesema Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania aliyeshika kijiti ameendeleza yale yote yaliyoanzishwa na Dkt. Magufuli na tumeshuhudia miradi mingi ikikamilika, mingine ikiwa katika hatua ya kuelekea ukamilifu na miradi mingi imeanzishwa kwa mwenendo ule ule na fikra zilezile kwa slogani yake kazi iendelee.
“Ni adhima ya Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu kuwaenzi viongozi wakuu wa kitaifa waliomtangulia na hatuna budi kuwaenzi viongozi hao kwa vitendo katika utendaji washughuli zetu, hivyo ni wasihi tuendele kumuombea ndugu yetu Hayati, John Pombe Magufuli na familia yake ikiongozwa na mama Janeth Magufuli”

“Tuendelee pia kumuombea Rais wetu wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuliongoza taifa kwa utulivu na amani kama tunavyoshuhudia sasa Tanzania imetulia kwa sababu Mkuu wa Nchi anafanya kazi kwa niaba ya Watanzania wote,” alibainisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amemshukuru mama Janeth Magufuli kwa jinsi alivyoweka utaratibu wa kumkumbuka Hayati John Pombe Magufuli lakini pia amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza misingi ya amani na utulivu.
“Tuendelee kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aendele kuliongoza taifa kwa utulivu, amani na maendeleo kama tunavyoshuhudia sasa Tanzania ikiwa imetulia,”alihimiza.
Naye, Askofu wa Jimbo katoliki Rulenge Ngara Mhashamu Severine Niwemugizi amesema Kanisa Katoliki lina utamaduni wa kuwakumbuka marehemu wote, ambao pia ni desturi ya kujifunza kutokana na maisha yao.
“Tunajua Hayati Dkt, Magufuli alipenda nidhamu katika utumishi wa umma na kuwajibika ikiwa ni pamoja na kukata mambo mabaya rushwa, unyanyasaji na uonevu hivyo tuandike kitabu chetu tukiwa tunaishi, ili tukimaliza kuandika kiwe na kurasa zenye mambo mazuri tuweze kujifunza na yale mambo mabaya tuachane nayo,” alieleza.


“Miaka minne iliyopita alipotembelea hapa Chato alituahidi kama familia kwamba hata tuacha na leo tunashuhudia uaminifu wake katika kutekeleza ahadi zake,” alisema Bi. Jesca.