TAKUKURU yakunjua makucha Jimbo la Kigamboni, yaanza na hawa Kata ya Tungi

DAR-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Kigamboni mkoani Dar es Salaam imesema,katika kuendelea kutekeleza majukumu yake Machi 13,2025 iliopokea taarifa fiche kutoka kwa msiri kuwa kuna mwananchi anaitwa Habibu Mchange ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha,kwa taarifa walizo nazo ni miongoni mwa wanaotaka kutia nia ya kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Kigamboni katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 14,2025 na Joseph Holle Makungu ambaye ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke amefafanua kuwa,taarifa iliyopokelea ni kwamba Habibu Mchange ameandaa baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Tungi ili awagawie fedha kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya uchaguzi ya mwaka 2024 na kanuni za Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya kampeni kabla ya dirisha kufunguliwa.

Pia,kuahidi kutoa zawadi ambazo haziko kwenye ilani ya chama cha mapinduzi, kwa kuwa si mtekelezaji wa ilani ya chama kwa kuwa si kiongozi, si mbunge, si mwakilishi, na wala si diwani katika chama hicho kwa sasa kama kanuni ya 69 (6) kuhusu uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola inayosema,

"Ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada wakati wa uchaguzi unapokaribia ambayo ni Dhahiri ina lengo la kuwavutia wapiga kura isipokuwa Rais, Mbunge, Mwakilishi, na Diwani ambao wako madarakani."

Amefafanua kuwa,baada ya kupokelewa taarifa ilifanyiwa uchunguzi wa awali kwa kuzingatia sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007 iliyofanyiwa marejeo ya mwaka 2022 na wachunguzi walifika katika ofisi ya CCM Kata ya Tungi majira ya saa saba mchana na kufanya Surveillance na kuweza kubaini baadhi ya viongozi wa CCM walikubaliana kukutana pale majira ya saa nane kamili.

"Ila baadae muda ulibadilishwa na kuwa saa tisa alasiri kwa sababu walikuwa wanamsubiria Habibu Mchange. Majira ya saa tisa Alasiri baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Tungi waliingia ukumbini na baada ya muda mfupi gari aina ya kluger yenye namba T366 EBL iliwasili kwenye maegesho ya magari ya ofisi hiyo ya CCM na baadae iligundulika ndiyo iliyokuwa imembeba Habibu Mchange.

"Aidha baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Tungi waliokutwa katika ukumbi huo hawakutaka kutoa ushirikiano kwa Maafisa wa TAKUKURU.

"Hivyo Maafisa wa TAKUKURU waliondoka na viongozi hao kuelekea Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni kwa ajili ya mahojiano na wote waliweza kueleza kuwa kikao kile hakikua halali n akiliitishwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Tungi,Sebastian Kapela Mabula.Uchunguzi wa tuhuma hizi unaendelea.

"TAKUKURU inafuatilia kwa karibu wote wanaodaiwa kufanya kampeni mapema kwa kutoa rushwa kwa wapiga kura kwa Jimbo la Kigamboni na Tanzania kwa ujumla kama ilivyofanyika kwenye tukio hili;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news