DODOMA-Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO),Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema,shirika hilo lipo mbioni kuanzisha Mkoa wa TANESCO wa Njia ya Treni ya Umeme (SGR) ambao utakuwa na kazi moja tu ya kushughulikia njia ya treni hiyo ili kuondoa changamoto za kuzimika njiani.
Mhandisi Nyamo-Hanga ametoa kauli hiyo Machi 26, mwaka huu jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Shirika hilo katika kipindi Cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Amesema,hatua hiyo ni kufuatia changamoto zilizojitokeza awali za kukatika kwa umeme katika treni hiyo kipindi Cha awali treni hiyo ilipoanza safari zake.
"Changamoto zilizojitokeza awali kwenye treni ya SGR kuzimika njiani, ni kwa sababu tulikuwa ndio tumeanza uendeshaji wake na hivyo walikuwa na hatua nyingi za kujifunza kwa TANESCO na hata kwa upande wa SGR,kitu kinapokuwa kipya yumkini kinaweza kuleta shida kwa sababu ya ugeni wake,"amesema Mhandisi huyo.
Hata hivyo,amesema laini ya umeme ya SGR sasa ipo madhubuti na huduma ya usafiri wa treni inaendelea vizuri.
"Kama shirika,tutahakikisha SGR tunaichukulia kama mkoa ,kwamba tunaweka menejimenti na Utawala maalum kwa ajili ya mkoa huo...katika level za kitanesco,katika kila mkoa huwa tuna Meneja wa mkoa ambaye anakuwa na timu ya watu wengi kuanzia registration, mafundi,mpaka wahandisi kwa ajili ya kuangalia huduma ya umeme katika mkoa huo.
"Timu hiyo itakuwa na kazi ya kushughulika na SGR tu lengo ni kuhakikisha kwamba umeme katika uendeshaji wa treni unakuwa wa uhakika na imara."