DODOMA-Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)limesema limeanza ujenzi wa kujenga laini kubwa ya kilovoti 400 ambayo itabeba umeme kutoka Chalinze mpaka Zuzu jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga ameyasema hayo Machi 26,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Ni kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2026 na ndiyo itakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi za umeme ambazo zipo sasa.
“Kwa sasa tunao mradi ambao tumeanza kujenga kwa ajili ya kuwa na laini kubwa ambayo itabeba umeme kutoka Chalinze ili iweze kuleta mpaka Dodoma na ukifika Dodoma uingie kwenye Substion ya Zuzu ambayo ndiyo Substion mama katika mfumo wetu wa Gridi ya taifa,”amesema Mhandisi Gissima.
Mhandisi Gissima amesema kuwa,umeme huo ukishakuwepo kutakuwa na uhakika kwamba huo umeme unaotoka Julius Nyerere unaweza sasa wote kubebwa na ukafika Dodoma na ukasambazwa kwenda kwenye maeneo yote ya nchi kwa kadri ya mahitaji ya matumizi.
Amesema kuwa,mradi huo umefadhiliwa na serikali ya Tanzania na umeanza kutekelezwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita na hadi sasa umefikia asilimia 15.
Vilevile,Mhandisi Gissima amesema kuwa, wana mradi wa kuunganisha Gridi ya Taifa na gridi ya mataifa jirani ili kuwa na kapu la pamoja la umeme.
“Gridi yetu na Kenya imeungana maana yake ni kwamba mfumo wetu wa umeme utaungana na nchi nyingi ambazo zipo katika ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Bara la Afrika.Kwa maana ya Kenya yenyewe kwenda Ethiopia, Sudani ya Kusini kwenda Uganda na kadhalika,”amesema.
Aidha, amesema kuwa wana mradi mwingine ambao utaunganisha na mfumo wa Tanzania na mfumo wa gridi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zinitwa nchi za SADC.
“Na tunachotaka kufanya pale kuwa na kapu la pamoja ambapo mradi huu umeanza kuanzia Iringa,miundombinu mikubwa ya umeme ya kilovoti 400 inajengwa kutoka Iringa mpaka Mbeya,Mbeya hadi Tunduma halafu Tunduma inavuka kwenda Zambia ukishafika Zambia tunajiunganisha na Gridi ya nchi za SADC.
“Mradi huu umeshaanza Km 624 zitajengwa lakini pia utekelezaji wake umefikia asilimia 34 ba mradi huu unapofika pale Tunduma maana yake tutairefusha ile laini ya msongo wa kilovoti 400 ili iweze kwenda Sumbawanga na baada ya hapo Mkoa wa Rukwa nao uweze kuingia kwenye mfumo wa gridi ya taifa na tunatarajia hili litakamilika mwaka 2026 hadi 2027,”amesema Mha.Gissima.