VIENNA-Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, Vienna, Mhe. Naimi Aziz anatarajiwa kuhutubia na kuwasilisha taarifa kuhusu utekekelezaji wa Sera ya Dawa za Kulevya na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Ni kwenye Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Kupambana na Dawa za Kulevya unaofanyika jijini Vienna, Austria kuanzia Machi 10 hadi 14,2025.
Mkutano huo unaohudhuriwa na Mawaziri na Wawakilishi kutoka nchi mbalimbali wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Dawa za Kulevya, unajadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili utekelezaji wa Mkataba huo.


Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unajumuisha wawakilishi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bohari Kuu ya Dawa, na Wizara ya Katiba na Sheria.