DAR-Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel William Shelukindo, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Ofisi za Umoja wa Mataifa za Huduma za Miradi (UNOPS), Bw. Rainer Frauenfeld, aliyefuatana na ujumbe wake.

Amesisitiza kuwa, Tanzania inathamini mchango wa UNOPS katika sekta mbalimbali, hususan miundombinu ya barabara na huduma za kijamii, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Balozi Shelukindo ameweka bayana dhamira ya Serikali kuendelea kushirikiana na UNOPS ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inazidi kuleta tija na kuendana na vipaumbele vya maendeleo vya Taifa.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utekelezaji wa miradi kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Bw. Frauenfeld ameipongeza Tanzania kwa kuwa moja ya nchi zinazotekeleza vyema vipaumbele vya Umoja wa Mataifa, hususan katika kuboresha huduma za kijamii.

Katika hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano huu, UNOPS imefungua rasmi ofisi yake nchini Tanzania.
Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kurahisisha usimamizi wa shughuli zake, na kuimarisha ushirikiano wa karibu na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo.