DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mpya wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Nicole Providoli, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam ambaye alifika kujitambulisha.
Katika kikao hicho walijadili masuala kadhaa ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Switzerland, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi hiyo, ukiwemo mradi wa kusaidia kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambapo tangu mwaka 2023, Uswisi imechangia shilingi bilioni 88.1 katika Mfuko huo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melkzedeck Mbise, Afisa Program-Utawala - kutoka Ubalozi wa Uswisi, B. Jacquiline Ngoma, na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Lisa Kilua.