Tuendelee kutenda mema na kudumisha amani nchini-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha wananchi kuyatenda mambo yote mema walioyatekeleza wakati wa Ramadhani ikiwemo ibada pamoja na kuiombea nchi amani ikielekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba,mwaka huu.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Machi 31,2025 alipozungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amezihimiza mamlaka zinazosimamia sheria za usalama barabarani kuzisimamia ipasavyo ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika katika kipindi cha Sikukuu ya Idd El Fitri.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,wakati wa sikukuu harakati za usafiri wa vyombo vya moto huongezeka barabarani, hivyo mamlaka zina wajibu wa kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara kwa kusimamia sheria kikamilifu.

Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa,ni vyema usalama wa watoto ukaimarishwa katika Viwanja vya Sikukuu ili wananchi washerehekee Sikukuu kwa Furaha na Amani kwa kudhibiti viashiria vyote vya udhalilishaji na uvunjifu wa amani.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuendeleza mwenendo wa kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali wakiwemo Watu wenye Ulemavu, Wajane,Wazee,Yatima na Watu wanaoishi katika Mazingira Magumu kwa kuwapa sadaka kwa kiwango kilichooneshwa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amewashukuru waumini wasio Waislamu kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Waislamu wakati wa Mwezi wa Ramadhani kuwa ni kielelezo cha ustahamilivu kwa waumini wa madhehebu tofauti jambo alilolisisitiza kudumishwa kwa manufaa ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news