DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameihimiza Jumuiya ya Khidmatul Tajwiid inayoandaa Mashindano ya Quraan Tajwiid kufanya juhudi za kuifikisha fani hiyo katika wilaya na mikoa yote nchini ili kupanua fursa na kuibua vipaji vya usomaji wa Quraan kwa Tajwiid.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipozungumza katika fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya Quraan Tajwiid yalioandaliwa na taasisi hiyo katika Ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam leo Machi 15, 2025.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema kufanya hivyo kutajenga jamii bora yenye maadili na tabia njema hususani kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Ameishauri jumuiya hiyo na nyingine za kidini kuzidisha juhudi zao kuwalea vijana na kuwaongoza kwenye maadili na ustawi wao.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amebainisha kuwa jukumu la kuwalea vijana sio la Serikali pekee bali kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kutoa ushirikiano kuhakikisha inajengwa misingi bora ya maadili na uchamungu ili kuwa na Taifa lenye hofu ya Mwenyezi Mungu.
Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa,kazi ya kusomesha Quraan ni kazi tukufu yenye malipo makubwa na mwenye kufanya kazi hiyo ni mtu bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.