ZANZIBAR-Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA),Juma Burhan Mohamed amesema,wana kila sababu ya kuwawezesha vijana ili waweze kuajirika na kujiajiri.
Ndugu Mohamed ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya hafla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano kati ya ZEEA na Taasisi ya Commonwealth of Learning yenye makao yake makuu nchini Canada.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Taasisi ya ZPDB, Maji House huko Mjini Magharibi Unguja.
Katika mazungumzo hayo, Juma Burhan Mohamed amesema kuwa,makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha vijana kupata elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kujiajiri na kuajirika.
Amesisitiza kuwa, ushirikiano huu ni hatua muhimu katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya ajira, hasa kwa vijana ambao hawakupata fursa ya elimu rasmi, lakini wana uwezo mkubwa wa kujifunza elimu ya amali, pamoja na wahitimu wa vyuo vikuu wanaohitaji ujuzi wa kiutendaji ili kuingia katika soko la ajira.