NA GODFREY NNKO
TAFITI mbalimbali zinaonesha kuwa, dawa za kulevya zina madhara makubwa ambayo yanaweza kuathiri sehemu nyingi za maisha ya mtumiaji na jamii kwa ujumla.
Ndiyo maana, wataalamu wanapendekeza kuzuia matumizi yake kwa kupitia elimu, msaada wa kisaikolojia na huduma za matibabu kwa wale walioathirika ili kuokoa kizazi kijacho.
Mfano Dkt. Nora Volkow ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya ya Marekani (NIDA) anasema kuwa, "Dawa za kulevya ni tishio kubwa kwa afya ya akili na mwili wa binadamu.
"Zinaathiri mfumo wa ubongo, zinaathiri kumbukumbu, uwezo wa kujifunza, na mwelekeo wa kufanya maamuzi."
Kwa upande wake,Dkt. Bruce Perry ambaye ni mtaalamu wa afya ya akili na mtindo wa utambuzi, anaeleza kuwa: "Watoto na vijana wanapozitumia dawa za kulevya, wanapoteza fursa za kujenga uwezo wao wa kiakili na kihemko.
"Jambo linalowaweka kwenye hatari ya matatizo ya kiafya na kisaikolojia kwa maisha yao yote.".
Naye mtaalamu wa afya ya akili, Dkt.Michael Miller anasisitiza kwamba, "Dawa za kulevya zina athari kubwa kwa afya ya akili, na zinaweza kuharibu uwezo wa ubongo kufanya kazi vizuri, jambo linalosababisha matatizo ya hisia na uhusiano."
Kuhusu malezi
Je? Malezi bora kwa watoto yaweza kusaidia udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika jamii?.
Katika kujibu swali hili, baadhi ya watumishi wa Mungu wanakiri ndiyo inawezekana, lakini pia wanashauri kuwa wazazi wawe mstari wa mbele kuwaongoza watoto wao katika nyumba za ibada.
"Inawezakana tena kwa asilimia zaidi ya 100, kinachotakiwa ni hao wazazi kuongozana na watoto wao katika nyumba za ibada, wasiwe wanawaacha watoto kwenda makanisani au misikitini huku wao wakibaki nyumbani.
"Kwenye nyumba za Mungu, kila anayefika lazima apate faraja, apate neno lenye kumjengea hofu ya kuyachukia matendo mabaya kama hayo matumizi au biashara za dawa za kulevya na kumjua Mungu.
"Kwa hiyo, tiba kuu dhidi ya malezi mabovu ambayo yanawafanya wengi hasa watoto kujiingiza katika matendo hatarishi kama matumizi ya dawa za kulevya ipo kanisani,"anafafanua Rais wa Mitume na Manabii Tanzania, Dkt.Joshua Mwantyala.
Naye Shehe Hassan kutoka Kisemvule ikiwa ni eneo kiunganishi kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani anasema kuwa,watoto na Watanzania bila dawa za kulevya inawezekana.
"Inawezekana si tu kwa sababu sisi wazazi au walezi tunajua kuchapa na kuwakoromea sana watoto, hapana ni kwa kuwatanguliza mbele ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na hakika hakuna kitakachomshinda."
Pia, Shehe Hassan anatoa pongezi kwa DCEA kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za dawa za kulevya.
"Na,elimu ni muhimu sana, binadamu tuna tabia ya kujisahau lakini, kadri elimu inavyokuingia basi inakuwa rahisi kuachana na yale maovu na kwenda katika mstari mnyoofu."
Wazazi wanasemaje?
Kwa upande wao wazazi Khamis Mohamed, Bhoke Julius, Matiko Matiko na Bahati Elias wakazi wa Kivule Fremu Kumi jijini Dar es Salaam wanasema kuwa,vita dhidi ya dawa za kulevya si vya kuiachia mamlaka pekee.
Wamesema, changamoto iliyopo kwa sasa mitaani ni baadhi ya makundi ya watu kuvuta bangi hata mbele za watoto, jambo ambalo wanasema kuwa, linafaa kuvaliwa njuga na wazazi wote.
"Hatupaswi kuoneana haya, kama ndani ya jamii kuna mtu au kundi la vijana linajihusisha na dawa za kulevya basi tuwaripoti, tusifichiane maovu, watoto wetu watakufa kwa dawa za kulevya."
Watoto na dawa za kulevya
Kuhusu ishara ya mtoto aliyepo katika hatari ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, Afisa Elimu Jamii kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Said Madadi anasema kuwa, mtoto anakuwa na viashiria mbalimbali.
"Kwanza kabisa mtoto aliyepo katika hatari ya kujiingiza kwenye dawa za kulevya, ni makundi yasiyoeleweka.Yaani kuwa na marafiki au makundi ambayo kwa mzazi akiyaangalia hayaeleweki."
Said Madadi anatolea mfano kuwa ni mtoto kuwa na marafiki ambao haukuonana nao kabla au kuwa na marafiki ambao ukiwaangalia unawatilia mashaka kwa muonekano.
"Maana yake kwa maana ya mavazi,lakini kuzungumza kwao na nyendo zao kwa ujumla."
Madadi anasema hiyo ni ishara ya kwanza ya mtoto ambaye yupo kwenye hatari ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine anabainisha kuwa, ni pale ambapo inajitokeza mtoto anakuwa na tabia ya usiri nyumbani ambayo awali haikuwepo.
"Mtoto akianza kutumia dawa za kulevya, au akiwa ana watu wanaomshawishi au akipewa kitu kigeni maana yake dawa za kulevya kwake ni kitu kigeni.
"Kwa hiyo,huwa anatabia ya kuwa msiri msiri, kwa taarifa ni kwamba utumiaji wa dawa za kulevya mara nyingi huendana na usiri au vitisho.
"Kwa hiyo, huwa anaweza akaambiwa asiseme, au anaweza akawaona watu wanatumia halafu akawaona, wakamwambia kwa sababu umetuona ukitutaja tutakufanya hivi...kwa hiyo, kuna usiri fulani."
Afisa Elimu Jamii huyo wa DCEA anasema kuwa, mtoto akianza kutumia huwa hakai karibu na wazazi kwa kuhisi anaweza kusikika hususani harufu yake.
"Au kutokana na athari ambazo zinamletea akitumia."
Jambo lingine amesema, ni pamoja na udokozi ndani ya nyumba.
"Kwa mfano ulikuwa unaweka hela, na hela zilikuwa zinakaa muda mrefu, lakini zikianza kudokolewa kidogo hicho ni kiashiria kimoja wapo.
"Kwa sababu hela unayompa inawezekana haimtoshelezi kula na kufanya vitu vingine.
"Inawezekana mzazi unampa shilingi mia tatu, ale shuleni lakini atakula, atakapotaka kutumia hizo dawa au kununua hivyo vitu, kwa hiyo anajikuta analazimika awe na ziada."
Udokozi
Kuhusu juu ya namna huyo mtoto atakavyopata hiyo ziada, Said Madadi anasema, ndipo hujikuta anaanza kudokoa taratibu.
Anasema, mtoto huyo anaweza akaiba vitu kwa ajili ya kwenda kuuza au akawa anadokoa.
Vilevile anasema, mtoto huyo anaanza utoro licha ya awali kuwa na tabia ya kwenda shule vizuri.
"Kwa hiyo, suala la utoro...utoro shuleni, hicho ni kitu cha kumwangalia pia mtoto wako."
Shida ya maumivu
Ishara nyingine, Madadi anasema ni kwa muonekano. "Mtoto ambaye anatumia dawa za kulevya, kwanza siku za mwanzo atakuwa na shida ya maumivu sana hasa ya kichwa."
Pia, ameeleza kuwa, mtoto huyo atakuwa na shida ya kukosa usingizi akiwa ameanza kutumia dawa za kulevya.
"Lakini, kingine akiwa ameanza kutumia harufu aidha ya jasho, analotoa kwa mfano anatumia labda bangi hiyo ni sifa kubwa inatokea."
Mbali na hayo, Afisa huyo anasema ishara nyingine ni kuwa na hasira. "Mtoto ambaye amekwishakuwa anaanza kutumia ana sifa hiyo, kwa sababu kama anatumia bangi huwa ina sifa ya kumpa ujasiri."
Kwa hiyo, anasema mtoto huyo anaweza kukujibu vitu ambavyo hautegemei kujibiwa.
Kuwa rafu
Ishara nyingine anasema ni kuwa rafu, kwani mtoto huyo hawezi kujijali tena kama mwanzo alivyokuwa anajijali kimuonekano.
Amesema, mtoto akianza kutumia tu kidogo dawa za kulevya kuna vitu anakuwa havifanyi tena.
"Lakini, kingine tabia ya uongo, hivyo ni vitu ambavyo ni miongoni mwa ishara ambazo mtoto anaweza kuwa kwenye hatari ya vitu kama hivyo."
Njia za kumfundisha
Kuhusu njia gani za kumfundisha mtoto kuhusu madhara ya dawa za kulevya, Said Madadi anasema kuwa, inategemea mtoto ana umri gani.
"Akiwa mtoto wa shule ya msingi au mdogo kwa kawaida hatumfundishi dawa nyingi za kulevya."
Anasema kwa kawaida huwa wanampa elimu ya athari za sigara na pombe.
"Kwa sababu hii ni milango ya kuingilia kwenye dawa ngumu (hard drugs), kwa hiyo unaweza ukaanzia hapo kwanza kumuambia athari zake."
Lakini, Madadi anasema kuwa, elimu hiyo inaweza ikaingia kwa kumuambia athari za sigara na pombe.
"Lakini, unaviweka mbali hivyo vitu, asiwe anaviona wakati wote. Mtoto ana tabia ya kujaribu kitu hicho."
Madadi anasema, jambo lingine katika rika ni kuangalia ikiwa umri wake ni shule ya msingi hapaswi kufundishwa sana kuhusu Cocaine ama Heroin.
"Utamuambia tu sigara, pombe lakini bangi kama anaiona ona, mtoto mwenyewe anakuwa mtaani sana."
Madadi anaongeza kuwa, mtoto huyo akiwa amesogea darasa la saba na kuendelea unaweza kumuongezea elimu ya bangi ingawa inapaswa ioneshe athari zaidi.
"Kuliko namna ya kutumia, kwa mfano madhara ya kuumwa, labda saratani, kama koo, madhara ya kupoteza viungo, madhara labda ya kuwa chizi."
Anasema, hivyo ni vitu ambavyo mtoto anatakiwa kuambiwa ili aogope kutumia ikiwa ndiyo uhalisia.
"Kwa mfano, bangi ina sifa hiyo ya kuharibu akili kwa sababu ya kemikali iliyopo ya THC (Tetrahydrocannabinol)."
Ushirikiano
Kuhusu aina za ushirikiano kati ya wazazi,shule na jamii unavyoweza kusaidia kumkinga mtoto dhidi ya dawa za kulevya amesema kuwa, wao mamlaka wanatoa elimu.
Pia, amesema katika kutoa elimu huwa wanafika mpaka shuleni na wanasisitiza shuleni zimeanzishwa klabu za kupinga rushwa.
"Lakini, sasa hivi zimejumuishwa klabu hizo na kupinga matumizi ya dawa za kulevya. Kwa hiyo, kwenye eneo hilo maana yake njia nzuri ni mtoto kumuingiza kupata hizo study, ajifunze hizo study za maisha.
"Lakini, vilevile kwenye hizo klabu wanafundishwa namna ya kuepukana aidha na makundi, lakini pia na matumizi."
Sababu za kufanya hivyo, Said Madadi anasema ni kufikisha elimu kuhusu dawa za kulevya kwa mapana na walimu wa malezi watatoa usaidizi.
"Sisi tunaweza kumshauri mzazi kuwa karibu na walimu, yaani usiamini kuwa mtoto anaweza akafanya kila kitu mwenyewe hata akiwa na umri gani.
"Ikiwa ni mwanafunzi, njia nzuri za kukaa naye ni kutengeneza mahusiano kati yako wewe na mtoto, lakini na walimu.Jitahidi sana, hata ikitokea kuna issues ambayo imeripotiwa shuleni, mzazi unaitwa kwanza usipinge.
"Kuonesha ushirikiano kwa walimu kuna vitu utavijua, kwa kwa sababu mtoto anapopata uhuru wa kuwa mbali na nyumbani, anapokuwa katikati ya nyumbani na shule, mara nyingi huweza kufanya matukio mengi au akaiga mengi, akayaona mengi.
"Kwa hiyo,kubadilika tabia hawezi kuonesha nyumbani ataonesha shule kwa sababu ya marafiki walioko shuleni.
"Kwa hiyo, jitahidi sana kuwa karibu na walimu hasa mwalimu wa darasa na walimu wa malezi pamoja na nidhamu, watakuambia mambo mengi juu ya huyo mtoto."
Marafiki wa mtoto
Said Madadi anasema, pia mzazi anapaswa kuwajua marafiki wa mtoto wake shuleni, kwani watamsaidia kuzijua tabia.
"Wewe utajua ni aina gani ya marafiki ni wazuri kukaa na mtoto.Kwa hilo ndiyo jambo kubwa."
Pia, Afisa huyo anatoa wito kwa wazazi kuwafundisha watoto kuepuka vitu kwa watu wasiowajua.
"Mfano madereva wa magari kumpa lifti, au madereva wa bodaboda awe makini sana kwenye maeneo hayo, mtoto unaweza kumkinga."
Jambo lingine amesema kuwa, ni mzazi kuwa karibu na mtoto hata akiwa nyumbani,kwani anaweza akaeleza shida ama matatizo yanayomsibu.
Anasema kuwa, ukiwa karibu zaidi na mtoto utamjua anapokuwa na mabadiliko, lakini pia ukiwa na jambo pale unapomfanya kuwa rafiki atakueleza changamoto anazopitia."Kwa hiyo ni rahisi mtoto kumuepusha."
Mafunzo
Kuhusu mafunzo au programu za kinga zinazopatikana kwa watoto na familia zao, Said Madadi anasema zipo, kwani mamlaka huwa inatoa elimu.
Amesema kuwa, huwa wanatoa elimu kwenye makundi mbalimbali ambapo miongoni mwao ni pamoja na familia.
"Ikitokea una uhitaji kama familia, unaweza ukamuita mtaalamu kutoka mamlaka atakusaidia."
Lakini, pili anasema kuwa,huwa wanatoa elimu zaidi kwenye maonesho yote ya Kitaifa na shughuli mbalimbali.
"Tatu, unaweza kushawishi kwenye shule kama kuna matukio hayo makubwa au kuna trends za watu kutumia dawa za kulevya, yanakuwa hatari kwa watoto, unaweza kwenda kushawishi kwenye vikao vya shule au ukawafuata waalimu.
"Kisha ukapata mawasiliano kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ikaenda katika eneo hilo kutoa elimu, kisha ikaanzisha klabu ikiwa hazijafikiwa."
Ameongeza kuwa, mtu anaweza kuwasiliana na watu wa mamlaka wakamsaidia ikiwa kuna hatua au mabadiliko kwa mtoto.
"Lakini, kama mtoto ana mabadiliko kubwa ni elimu ambayo inatolewa, kwa hiyo kuna elimu ya familia kwa wazazi kujua dawa za kulevya ni nini, madhara yake,tabia na mambo gani ya kuepuka."
Hatua za kuchukua
Hatua ambazo wazazi wanapaswa kuchukua ikiwa watagundua mtoto ameathiriwa na dawa za kulevya, Said Madadi anasema baada ya kuzijua dalili za usiri, kiburi, hasira, majibu ya hovyo, wizi, utoro shuleni, kuwa rafu ambazo ni dalili za awali.
"Lakini, ukimfuatilia vizuri utamg'amua ukimkagua vitu vyake mara kwa mara akiwa hayupo au kwa kumshtukiza, utamgundua.
"Sasa basi,ukishamgundua mtoto wa aina hizo mpeleke kwanza hospitali wakampime, hospitali zetu zina vipimo vya kuonesha sampuli."
Amesema, baada ya vipimo itaonesha ni aina gani ya dawa za kulevya mtoto anatumia.
"Ukishagundua unaweza ukaanza matibabu, lakini pili tunazo asasi zetu ambazo huwa tunafanya nazo kazi kwa pamoja.
"Inawezekana eneo ulilopo ni mbali, ukitoa taarifa tunaweza tukakuunganisha na watu wao wakamsaidia mtoto."
Amesema, mtoto akiwa tayari ameathirika kwa dawa za kulevya anapaswa kupata tiba mara moja.
"Sasa, tiba inategemea ni aina gani ya dawa za kulevya ambazo ametumia."
Amesema, kama mtoto huyo ametumia Heroin ni lazima atakwenda kwenye vituo vya MAT ili apate msaada wa dawa aina ya Methadone.
Pia, kama ametumia dawa zenye asili ya afyuni atatumia dawa aina ya Methadone.
Taarifa zinasemaje?
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2023 iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), ilionesha kuwa, katika maeneo mengi duniani, kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Mfano katika taarifa hiyo ilionesha kuwa mwaka 2021, takribani mtu mmoja kati ya kila 17 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64 duniani alitumia dawa za kulevya katika kipindi cha mwaka uliopita.
Idadi iliyokadiriwa ya watumiaji wa dawa za kulevya kwa miaka kumi imeongezeka kutoka milioni 240 mwaka 2011 hadi milioni 296 mwaka 2021 ambalo ni ongezeko la asilimia 23.
Katika kipindi hicho,dawa za kulevya kama bangi, heroin, metamphetamine, cocaine pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya zilitumika.
Mwaka 2020, ilikadiriwa kuwa watu milioni 36 walitumia dawa za kulevya jamii ya amphetamine (ATS), milioni 22 walitumia cocaine, na milioni 20 walitumia dawa aina ya “ecstasy”.
Wanawake walitumia ATS zaidi na dawa tiba zenye asili ya kulevya wakati wanaume walitumia zaidi dawa jamii ya afyuni na cocaine.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa,katika kipindi hicho, kulishuhudiwa ongezeko kubwa la uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa mpya za kulevya (New Psychotropic Substances-NPS) kuwahi kutokea duniani.
Matumizi ya dawa za kulevya yaliripotiwa kusababisha madhara ya kiafya kwa watumiaji na jamii, kama vile ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI, magonjwa ya akili na homa ya ini.
UNODC
Wakati huo huo,Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Kukabilia na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) linabainisha kuwa,kuibuka kwa dawa mpya za kulevya za kutengenezwa na rekodi ya usambazaji na mahitaji ya dawa zingine kumeongeza athari za dawa hizo.
Vilevile,hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa shida za utumiaji wa dawa za kulevya na madhara kwa mazingira.
Hayo yameainisha katika Ripoti ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2024 ambayo inabainisha kuwa,idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya duniani imeongezeka na kufikia watu milioni 292 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 katika kipindi cha miaka 10.
Akizindua ripoti hiyo mwaka jana jijini Vienna nchini Austria, Mkurugenzi Mkuu wa UNODC, Ghada Waly ameeleza kuwa,uzalishaji wa dawa za kulevya na matumizi yake unazidisha ukosefu wa utulivu na usawa wakati huo huo ukisababisha madhara makubwa kwa afya, usalama na ustawi wa watu.
“Tunahitaji kutoa matibabu yaliyofanyiwa uchunguzi na kuwa na ushahidi wa kuweza kusaidia wale walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya huku tukilenga soko haramu la dawa za kulevya na kuwekeza zaidi katika kuzuia matumizi ya dawa hizo.”
Waly anabainisha kuwa,matumizi ya bangi yamesalia kutumika zaidi duniani kote ambapo kuna watumiaji watumiaji milioni 228, ikifuatiwa na dawa nyingine ambazo ni opioids yenye watumiaji milioni 60.
Kwa upande wa amphetamines ina watumiaji milioni 30, cocaine watumiaji milioni 23, na ecstasy ikiwa na watumiaji milioni 20.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwekwa rekodi mpya ya juu ya uzalishaji wa cocaine tani 2,757 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 zaidi tangu mwaka 2021.
Aidha,ripoti hiyo inabainisha kuwa,ingawa wastani wa watu milioni 64 duniani kote wanakabiliwa na matatizo yatokanayo na matumizi ya dawa ya kulevya, ni mtu mmoja tu kati ya 11 anayetibiwa.
Pia,wanawake wanapata huduma ndogo zaidi za matibabu ikilinganishwa na wanaume.
Kwani,ni mwanamke mmoja tu kati ya 18 mwenye matatizo ya matumizi ya dawa za
kulevya ndio anapata matibabu ikilinganishwa na mwanaume mmoja kati ya saba.
Kwa mujibu wa utafiti huo wa mwaka 2022, inakadiriwa kuwa watu milioni saba walikamatwa au kupewa onyo au tahadhari na polisi kwa makosa ya matumizi ya dawa za kulevya, na karibu theluthi mbili ya jumla hiyo kutokana na matumizi ya dawa za kulevya au kupatikana kwa matumizi.
Aidha, watu milioni 2.7 walifunguliwa mashitaka kwa makosa ya dawa za kulevya na zaidi ya milioni 1.6 walitiwa hatiani duniani kote mwaka wa 2022, ingawa kuna tofauti kubwa katika kanda mbalimbali za Dunia kuhusu mwitikio wa haki ya jinai kwa makosa ya dawa za kulevya.
Matibabu
Ripoti hiyo imeeleza jinsi haki ya afya ni haki ya binadamu inayotambulika Kimataifa ambayo ni ya binadamu wote, bila kujali hali ya mtu kutumia dawa au kama mtu kuwekwa kizuizini au amefungwa.
UNODC inasema haki hiyo inatumika sawa kwa watu wanaotumia dawa za kulevya, watoto na familia zao, na watu wengine katika jamii zao hivyo nchi zinapaswa kuheshimu na kutekeleza haki hiyo kwa watumiaji wa dawa za kulevya.
Katika athari nyingine kwa jamii UNOCD imesema, wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameingilia katika nyanja nyingine za kiuchumi ambazo ni haramu ikiwemo usafrishaji wa wanyamapori, ulaghai wa kifedha na uchimbaji haramu wa rasilimali.
Jamii za wakimbizi, wahamiaji na watu masikini wamejikuta matatizoni,kwani wamekuwa wakilazimishwa kugeukia kilimo cha Opium au uchimbaji wa rasilimali haramu ili kuweza kuishi.
Aidha, jamii hizo pia zimejikuta zikitumbukia katika mtego wa madeni na vikundi vya uhalifu au wao wenyewe kutumia dawa za kulevya.
Shughuli hizi haramu pia zinachangia uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti, utupaji wa taka zenye sumu na uchafuzi wa kemikali.
Hata hivyo, jitihada mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kudhibiti uzalishaji, biashara, na matumizi ya dawa zakulevya, ikiwa ni pamoja na utoaji wa tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa hizo.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Makala
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)