Uchumi wa Tanzania wazidi kuimarika, Gavana Tutuba abainisha mengi

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa,hali ya uchumi wa Tanzania imeendelea kuimarika na kuwa himilivu.
"Mpaka sasa, Tanzania imeendelea kung'ara katika medali za kiuchumi kidunia. Hali yetu ya uchumi, imeendelea kuwa nzuri katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Fedha ambayo imeendelea kuimarika, imeendelea kuwa na utulivu, imeendelea kuwa thabiti.

"Imeendelea kuwa na mtaji mkubwa na ukwasi wa kutosha na pia ina ufanisi mzuri wa viwango vya kimataifa na inajiendesha kwa faida na inaendelea kukuwa kwa kasi nzuri;

Gavana Tutuba ameyasema hayo Machi 20,2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa wananchi na wadau mbalimbali.

Hafla kama hiyo pia, imefanyika makao makuu ya BoT jijini Dodoma, makao makuu ndogo Zanzibar, matawi ya Mtwara, Mwanza,Arusha na Mbeya.
Amesema, kwa kipindi cha miaka mitatu Sekta ya Uchumi na Fedha nchini imeendelea kufanya vizuri.

"Na kwa takwimu tunafahamu kwamba, kwa mwaka 2024 uchumi wa nchi yetu ulikuwa kwa takribani asilimia 5.4 ikilinganishwa na ukuwaji wa uchumi wa kidunia ambao ulikuwa asilimia 3.2.Kwa hiyo tumefanya vizuri."

Aidha, kwa upande wa mfumuko wa bei, Gavana Tutuba amesema ulikuwa asilimia 3.1 ukilinganishwa na mfumuko wa bei wa kidunia wa asilimia 4.7.

Mikopo

Kwa upande wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, Gavana Tutuba amesema, mambo yalikuwa mazuri, kwani likuwa kwa asilimia 16.8 ikilinganishwa na lengo la asilimia 15.

"Lakini, pia kwa upande wa mikopo chechefu tumeendelea kufanya vizuri ambapo kiwango cha mikopo chechefu kwa mwaka 2024 ilikuwa asilimia 3.3 ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika kimataifa cha asilimia 5.Kwa maana hapa nako tumefanya vizuri."

Vilevile Gavana Tutuba amesema, nakisi ya urari ya malipo nje ilipungua kufikia asilimia 2.7 ya pato la taifa kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 3.7 ya pato la Taifa kwa mwaka 2023.

"Akiba ya fedha za kigeni imefikia dola za kimarekani milioni 5.5 kiwango ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa miezi 4.7."
Mbali na hayo amesema, Pato la Taifa limeendelea kuwa himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Amesema, kwa mwaka 2024 ilikuwa takribani asilimia 41.1 pato la taifa kwa thamani halisi ya sasa.

Ukilinganisha na ukomo uliowekwa kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa asilimia 53.

"Kwa hiyo, takwimu hizi ni kiashiria tosha kwamba tunafanya kazi vizuri na Mwenyezi Mungu ameendelea kutubariki kama nchi ya Tanzania uchumi bado upo vizuri na tunaendelea vizuri."

Huduma za Kifedha

Gavana Tutuba amesema, katika kipindi cha karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la huduma za kifedha hapa nchini.

Amesema, ongezeko hilo limechangiwa na kasi, usimamizi mzuri wa Sekta ya Fedha pamoja na kuongezeka kwa watoa huduma ndogo za fedha hasa baada ya kupitishwa kwa sheria ya usimamizi wa huduma ndogo za fedha ya mwaka 2018.

Amesema, licha ya mafanikio hayo bado zipo changamoto chache zilizojitokeza katika sekta hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo katika huduma za kifedha,Gavana Tutuba amesema ni pamoja na utolewaji wa mikopo isiyofuata sheria (mikopo umiza au kausha damu).

Sambamba na wanaotoa mikopo yenye riba kubwa huku wengine wakitoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni.
"Wengine walikuwa wakitoa huduma hizo kwenye mitandao ikiwemo utapeli uliofanyika kwenye shughuli za upatu."

Kataeni upatu

Kutokana na changamoto hiyo, Gavana Tutuba ametoa wito kwa wananchi wote kujiepusha na shughuli za upatu.

Pia, amewataka wananchi kuhakikisha wanapata huduma za mikopo kwa watoa huduma wenye leseni halali kutoka Benki Kuu au kupitia taasisi zilizokasimishwa mamlaka.

"Kwenye halmashauri kwa leseni za VICOBA na kwenye Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa leseni za SACCOS."

Pia, amewataka watoa huduma za mikopo wenye leseni kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na ambazo haziwaumizi wananchi.

Amesema, kwa yule ambaye atakwenda kinyume na leseni yake, Benki Kuu itachukua hatua ikiwemo kumfutia leseni husika.

Kuhusu mfungo

"Kipindi hiki cha mfungo ninafahamu ni kipindi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Na Kipindi ambacho kina faida nyingi za kiroho na kimwili."

Gavana Tutuba amesema, kwa upande wa kiroho, viongozi wengi wa kidini zote za Kiislamu na Kikristo wameendelea kufundisha hiki ni kipindi muhimu ambacho mwanadamu anapaswa kumrejea Mungu wake.
"Ni kipindi ambacho kinatupatia fursa na Mwenyezi Mungu kwa sala, maombi na hata kutafakari ukuu wa Mwenyezi Mungu."

Pia, amesema katika kipindi hiki kila mmoja anapata fursa ya kutakasa roho na nafsi yake

"Lakini, tunaendelea kuongeza hamasa ya kusoma neno la Mungu, kumtafuta Mungu, kumsikiliza Mungu, kumtii na kumheshimu Mungu na pia kuzingatia amri na mafundisho yake."

Gavana Tutuba amesema, pia ni kipindi ambacho kinaleta mwamko wa kuishi maisha matakatifu ya hapa duniani huku kila mmoja akifuata mafundisho na kuangalia namna ya kubadilika ili tumrejee Mungu.

Mbali na hayo, Gavana Tutuba akizungumzia faida za kimwili katika kipindi hiki amesema, kufunga kuna faida nyingi.

Miongoni mwa faida hizo amesema, ni pamoja na kupunguza uzito na mafuta ambayo hayahitajiki mwilini.

Kufunga pia, Gavana Tutuba amebainisha kuwa, kunaimarisha afya ya moyo na kupunguza changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo ugonjwa wa saratani.

"Vilevile, kufunga kunaimarisha uwezo wa kumbukumbu, kwa hiyo kufunga kuna faida nyingi sana."

Wakati huo huo, Gavana Tutuba amewapongeza Waislamu na Wakristo wote kwa kuzingatia nguzo hiyo muhimu katika imani.

"Ninaomba pia, niendelee kuwasihi wote kwamba tuendelee kuyaheshimu mawaidha na mahubiri mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa dini katika kipindi hiki cha mfungo Mtukufu.

"Pia, tuendelee kumcha Mungu hata baada ya mfungo wa Ramadhani na Kwaresma.

"Tunafahamu katika maisha yetu ya binadamu tuna wajibu hasa wa kutumia kipindi hiki tunapofunga kwa wale ambao walikuwa na changamoto za mawazo mabaya, wafunge mawazo mabaya, wafunguwe mawazo mema.

"Walioko kwenye vita, wafunge vita au migogoro ili waweze kufungua amani, wingine walioko kwenye ugomvi wafunge ugomvi ili waweze kufungua upatanishi.

"Wengine wafunge dhuluma ili waweze kufungua haki, wengine wafunge chuki ili hatimaye wafunguwe upendo.

"Na wengine wafunge uongo ili wafunguwe ukweli,wengine wafunge wizi ili wafunguwe usalama na pia wengine wafunge hasira ili hatimaye wafunguwe furaha."
Aidha,Gavana Tutuba amewakumbusha washiriki wa futari hiyo kuwa siku ya leo Machi 20,2025 ni Siku ya Furaha Duniani.

Hivyo, amewahimiza kuwa kila mmoja anayo nafasi ya kujipanga ili kuhakikisha analeta furaha hapa duniani.

Amesema,matarajio yake ni kwamba katika kipindi hiki kitaendelea kuleta chachu ya kuimarisha amani, upendo na mshikamano kuanzia ngazi ya familia,Taifa hadi Kimataifa.

"Kwa hiyo, tuendelee kutumia kipindi hiki kujitafakari na kuangalia namna ya kumrudia Mwenyezi Mungu."

Pia, Gavana Tutuba amewahimiza kila mmoja kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kulinda amani iliyopo.

"Na tuendelee kuzingatia maelekezo ya viongozi na hata ikiwezekana ufanye kazi upate kipato kilicho halali.

"Tuendelee hata kulipa kodi na tozo stahiki za Serikali ili tupate maendeleo, pia tuendelee kuzingatia zile 4R za Mheshimiwa Rais anazoendelea kusisitiza yaani Maridhiano, Ustahimilivu, Kufanya Maboresho na Mabadiliko katika maisha yetu.
"Lakini, pia tuendelee kurejesha matumaini mema katika kulitumikia Taifa na hata kuongeza matumaini mapya pale ambapo kulikuwa na kukata tamaa na vilevile tuendelee kumrudia Mwenyezi Mungu ili naye aweze kutubariki zaidi.

"Tunafahamu kwamba, yapo mambo mengi sana tunapaswa kujifunza kutokana na kufunga kwa sababu kufunga pia ni sehemu ya sala na viongozi wengi wa dini wamekuwa wakituhimiza wakati tukiendelea kufunga tupate pia na fursa ya kutafakari neno la Mungu."

Mufti wa Tanzania

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally, ameitaka Benki Kuu kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya huduma za fedha.

Amesema, kupitia elimu ya fedha kwa wananchi itawapa uwanda mpana wa kuweza kutambua sehemu sahihi za kupata mikopo.

Pia, amesema elimu hiyo itasaidia wananchi kuendesha biashara zao kwa faida.

"Kwa hiyo msiache kutoa elimu hii, ili iweze kufikia mahali ambapo mwananchi anaweza kufanya shughuli zake kwa utulivu."
Pia,amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani nchini hasa kipindi hiki Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu."Kwa hiyo, Watanzania tushikamane tuitunze amani."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news