BRIGDETOWN-Tanzania imelenga kuunganisha nishati ya jotoardhi kwenye gridi ya taifa ifikapo mwaka 2030 ili kuwa na umeme wa uhakika unaotokana na nishati jadidifu kuelekea Dira ya Tanzania 2025 ambayo inasisitiza maendeleo endelevu ya nishati kama nguzo ya mabadiliko ya kiuchumi.

"Lengo letu ni kuunganisha nishati ya jotoardhi kwenye gridi ya taifa ifikapo 2030, Suala hili ni miongoni mwa azma yetu pana ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa wote ifikapo 2030 ili kuondokana na uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo 2050.
"Hii ni kutokana na Sera ya Taifa ya Nishati ya Tanzania 2015 yenye Mpango Mkuu wa Nishati 2020 pamoja na Tamko la Dar es Salaam la “Mission 300” katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa 2025,”amesema Mha. Mramba.
Mha. Mramba amesema kuwa, mikoa 16 nchini Tanzania itanufaika na maendeleo ya nishati ya jotoardhi, na kuifanya kuwa msingi wa mkakati wa nishati endelevu, Nia hii inajidhihirisha kupitia uanzishwaji wa Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa lengo la kutafiti na kuendeleza rasilimali za jotoardhi ambapo hadi sasa kampuni hiyo inafanya kazi katika maeneo zaidi ya 50.

Naye, Waziri wa Nishati wa Shirikisho la St. Kitts na Nevis, Mhe. Konris Maynard amesema kuwa nchi zinatakiwa ziwe tayari kukuza matumizi ya jotoardhi na kuhama katika katika matumizi ya nishati zisizo salama kwa mazingira.
Aidha amewataka wadau walioshiriki mkutano huo kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati ya jotoardhi.
Tanzania imebarikiwa kuwa na uwezo mkubwa wa nishati ya jotoardhi, unaokadiriwa kuwa zaidi ya 5,000 MW za umeme na 15,000 MW za nishati ya joto.
Vilevile, Tanzania ina bahati ya kuwa katika eneo la kijiografia ambapo kwa upande Mashariki na Magharibi imezungukwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki (EARS), hali hii inaifanya Tanzania kuwa na msingi wa kijiolojia unaofaa kwa ajili ya kutumia rasilimali hiyo Jadidifu.