Utii wa viongozi ni nguzo muhimu serikalini-Rais Dkt.Mwinyi

■Asema kukosekana kwa Utii wa Viongozi kumekuwa chanzo cha Fitna, Majungu na Mifarakano baina ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itahakikisha kunakuwepo kwa Utii wa Viongozi katika utendaji wa taasisi za umma ili kuepusha mifarakano baina ya watendaji.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza hayo leo alipozungumza katika Kongamano la Pili la Kiimani kwa Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililofanyika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni, Wilaya ya Mjini.

Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa, kukosekana kwa Utii wa Viongozi kumekuwa ndio chanzo cha Fitna, Majungu na Mifarakano baina ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,amekuwa akipokea taarifa nyingi za kuwepo kwa ugomvi katika taasisi za umma baina ya watendaji wenye dhamana jambo ambalo Serikali inadhamiria kuliondosha.

Akizungumzia suala la Utoaji wa Zaka amesema kuwa, ni suluhusho la umasikini miongoni mwa jamii pale zaka inapotolewa kwa usahihi na kuwafikia watu wenye uhitaji.
Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa,endapo zaka itatolewa kwa usahihi na kuifuata Miongozo ya Sheria za Kiislamu kundi kubwa la watu wangetoka katika dimbwi la umasikini.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali kwa kupitia Afisi ya Mufti Mkuu itaendelea kusimamia taasisi ili suala la ugawaji wa Zaka lifanyike kwa usahihi zaidi.
Akizungumzia kuhusu amani Dkt.Mwinyi amesema, ndio suala muhimu zaidi katika nchi na kila mmoja kwa nafasi aliyonayo anapaswa kuhubiri amani.

Dkt.Mwinyi amesema, kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapa Zanzibar kunalenga kudumishwa kwa amani na kuwasihi wanasiasa kushirikiana na Serikali kufanikisha azma hiyo kwa manufaa ya n̈chi.
Amesisitiza kuwa, nchi haipaswi kurudi nyuma katika mifarakano ya kisiasa,kwani kunachangia kuporomoka kwa uchumi na kushindwa kuleta maendeleo.

Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Afisi ya Mufti Mkuu kwa kusimamia vizuri na kuendeleza mambo yote ya Dini ya Kiislamu ikiwemo kongamano hilo la kiimani kwa viongozi wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news