VIDEO:Ghasia ndani ya CHADEMA,Mwenezi wa BAWACHA Taifa ashambuliwa na walinzi wa Heche

NJOMBE-Katika kile kinachoonekana kama mgawanyiko unaokua ndani ya CHADEMA, taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Siglad, alipigwa na walinzi wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche.
Tukio hilo lilitokea usiku wa jana mkoani Njombe, katika kikao cha ndani cha chama hicho.

Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya mabishano makali kuhusu masuala ya uongozi na mwelekeo wa chama, ambapo Siglad alionekana kutofautiana na mtazamo wa kundi linalomuunga mkono Heche.

Walinzi wake walidaiwa kumpiga kwa nguvu na kumdhalilisha, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa wanachama waliokuwepo.

Mpasuko unazidi kuonekana

Tukio hili linadhihirisha mpasuko unaozidi kujitokeza ndani ya CHADEMA, hasa kati ya viongozi wanao unga mkono kususia uchaguzi na wasio unga mkono kususia uchaguzi.

Mgawanyiko huu unaonekana kuchochewa na siasa za makundi ndani ya chama hicho, ambapo viongozi mbalimbali wanapambana kuonyesha ushawishi wao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Tayari baadhi ya wanachama wa CHADEMA wameanza kuhoji uhalali wa matendo ya walinzi wa viongozi wa chama kutumia nguvu dhidi ya wenzao.

Swali linalojitokeza ni je, kuna demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho au ni utawala wa mabavu kwa wanaokosoa baadhi ya viongozi?.
Wito wa Haki na Uwajibikaji

Wachambuzi wa siasa wanaona tukio hili kama ishara ya migogoro ya ndani inayoweza kudhoofisha CHADEMA katika maandalizi yake ya uchaguzi. 

Wanachama na viongozi wa chama wanapaswa kujitathmini ili kuhakikisha kuwa tofauti za kisiasa haziishii kwenye matumizi ya nguvu, bali zinatatuliwa kwa njia za kidemokrasia.

Hadi sasa, uongozi wa CHADEMA haujatoa tamko rasmi kuhusu tukio hili. Je, hatua gani zitachukuliwa dhidi ya waliohusika? Je, CHADEMA itaweza kudhibiti migogoro ya ndani na kuonyesha mfano wa demokrasia wanayoihubiri? Muda utaamua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news