KILIMANJARO-Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imefanya zoezi la kupanda miti kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji.
Mamlaka imekuwa na utaratibu wa kupanda miti rafiki ya maji kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo ya vyanzo vya maji, matenki na maeneo mbalimbali yenye uhitaji ili kuhifadhi uoto wa asili.
Aidha,kwenye maadhimisho haya mamlaka imepanda miti hiyo kwa kushirikiana na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Kilimanjaro ambapo tenki la kuhifadhi maji liko kwenye kata hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Philbert Nyangwe ametoa rai kwa wadau mbalimbali kujitokeza kupanda miti ili iweze kurejesha uoto wa asili kuhakikisha upatikanaji wa maji.
Akizungumza na waandishi wa habari,Bi. Florah Nguma ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma ameeleza kuwa,mamlaka itaendelea na Ofa ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kurejeshea huduma wateja waliositishiwa huduma bila faini na waliolipia nusu ya deni wanalodaiwa mpaka tarehe 31/3/2025.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka 2025 yamekuwa na Kauli mbiu isemayo Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji.