Vijana ni Jeshi Kubwa la Mama

DODOMA-Maelfu ya wanavyuo kutoka vyuo mbalimbali mkoani Dodoma wamefanya matembezi maalum kwa ajili ya kuweka maazimio kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.Matembezi hayo yamefanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Kampeni ya Mama Asemewe, Ndg. Geofrey Kiliba, yakihusisha wanachama wa kampeni hiyo wanaounga mkono juhudi za maendeleo za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya matembezi hayo, Ndg. Geofrey Kiliba alisema kuwa lengo la matembezi hayo ni kuonyesha mshikamano wa wanavyuo katika kuchagiza maendeleo ya taifa na kuandaa mikakati ya kuhakikisha vijana wasomi wanashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao.

“Tunatambua mchango wa vijana katika ustawi wa nchi yetu, na kupitia Kampeni ya Mama Asemewe tunajipanga kuhakikisha tunashiriki kikamilifu katika kujenga Tanzania yenye maendeleo endelevu chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Kiliba.
Katika maazimio yao, wanavyuo wameeleza dhamira ya kushiriki kwa wingi katika mchakato wa uchaguzi, kuhakikisha ushiriki wa vijana unakuwa na nguvu, na kuendelea kueneza uelewa kuhusu sera na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Matembezi hayo yamehitimishwa kwa Kongamano kubwa la Wanavyuo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, lililowakutanisha wanavyuo, viongozi wa kampeni, na wadau mbalimbali wa maendeleo. Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mh. Deogratius Ndejembi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo mipango zaidi iliwekwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Wanavyuo walisisitiza kuwa, kama kundi muhimu katika maendeleo ya taifa, wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa maendeleo yanayofanywa yanaeleweka kwa wananchi na kuwahamasisha vijana wenzao kushiriki kikamilifu katika michakato ya kidemokrasia ili kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news