DAR-Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha, likiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba limekutana leo tarehe 10 Machi 2025 katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam.

Kikao hiki kimewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya fedha kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayohusu usimamizi, uendelevu, na uimara wa sekta hiyo.
Katika mkutano huo, wajumbe wamejadili changamoto zinazoikabili sekta ya fedha, fursa za kuboresha mifumo ya usimamizi, pamoja na namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo.
Lengo kuu la majadiliano haya ni kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inabaki kuwa thabiti, shindani, na yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Miongoni mwa taasisi zilizohudhuria kikao hicho ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania; Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara ya Fedha Tanzania; Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar; Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI);

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA); Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA); Bodi ya Bima ya Amana(DIB); Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania; Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Tume ya Ushindani (FCC).