DAR-Wito umetolewa kwa Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Alama za Taifa ikiwemo Ngao ama Nembo ya Taifa, Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa na kuendelea kujifunza matumizi sahihi ya alama hizo pamoja na matumizi ya Gazeti la Serikali.
Hayo yamesemwa mapema leo Machi 20,2025 na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bw. George Lugome kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari jijini Dar es Salaam.
Bw. Lugome amesema kuwa hivi karibuni kumekuwa na upotoshwaji wa Alama za Taifa na kukumbusha kuwa Alama hizi zipo kwa mujibu wa sheria.
“Na yeyote atakayechezea alama hizi atapata adhabu kwa mujibu wa sheria na adhabu yake kwa yeyote anayekiuka atatumikia kifungo cha miaka miwili Jela ama faini,ama vyote viwili kwa pamoja, ambapo sheria hii ya mwaka 1964 ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa.” Alisisitiza.
Akizungumza kuhusu Nembo ya Taifa, Bw. Lugome alisema kuwa Nembo hiyo, ipo kwa Matumizi ya shughuli za Serikali pekee na sheria imesema Wazi, na aliongeza kwa kusema kuwa matumizi ya alama za Taifa ambayo siyo sahihi yanaharibu Haiba ya Taifa na Idara ya Mpiga Chapa ndiyo yenye jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa matumizi ya Alama hizi yanatumika kwa usahihi.
Aidha, Bwana Lugome alifafanua kuwa uchapishaji holela wa alama hizi na uchoraji wa nembo hizi kuonesha ubunifu wao, unachangia upotoshwaji na kuharibu uhalisia wake.
Kwa Upande wa Bendera ya Taifa, Bw. Lugome Alizungumza na kutolea ufafanuzi kuhusu rangi nne za Bendera ya Taifa zinazotumika
Akizungumzia Wimbo wa Taifa, Bw. Lugome alisema Wimbo wa Taifa Unavyoimbwa lazima uimbwe kwa beti zote mbili na kufuata Ala zilizowekwa na kusimama kikakamavu ambapo ni hali ya kuonesha utamaduni na Uzalendo kwa Taifa hili.
