NA GODFREY NNKO
KUELEKEA kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, wanawake kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wamewatembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wanawake waraibu wa dawa za kulevya katika Kituo cha Tiba Saidizi kwa Waraibu kwa kutumia Dawa (MAT).
Ni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ya leo Machi 7,2025 imeongozwa na Veronica Octavian Matikila ambaye ni Kamishna wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
"Leo tumeona ni vema tukasherehekea vilele hivi vya Sherehe ya Siku ya Wanawake Duniani pamoja na wanawake ambao ni waraibu wanaopata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke.
"Kwa nini tumeamua kuchagua hospitali hii? Ukiangalia katika mamlaka tuna misingi minne ambayo tunaifanyia kazi."
Kamishna huyo amesema,msingi mmoja wapo ni kuhakikisha wanasaidia kupunguza madhara ya dawa za kulevya.
"Tunapunguza madhara ya dawa za kulevya kwa kutoa tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya kwa kupata huduma katika hospitali kama MAT ambayo hiyo inapatikana katika Hospitali ya Temeke ikiwa ni kituo kimoja wapo kinachotoa huduma za Methadone.Lakini,kwa pamoja tunafanya kwa kupitia nyumba za upataji nafuu.
"Tumepata nafasi ya kukaa na kuongea nao,na wametuelezea ni historia gani ambayo iliwapelekea wao wakaanza kujiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya.
"Lakini, pia kuwarejeshea tumaini na imani kwamba Serikali inawathamini, inawapenda japo kuwa kama mamlaka tunapambana na tuko kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
"Hatuna nia ya kutokuwajali raia wetu, raia wa Tanzania wana thamani kwa hiyo kama wanawake tumekuja kuwatia moyo."
Pia amewataka kutambua kwamba,Serikali inawathamini na imewekeza kiasi kikubwa cha pesa kuweza kuwasaidia waweze kurudi katika hali zao za kawaida ili waweze kuwa pia na tija katika uzalishaji kiuchumi, lakini pia na thamani kijamii.
"Tunawaasa wanawake wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya msiogope, njooni Serikali imewekeza pesa za kutosha, imeweka utaratibu wa kutosha kuweza kuwasaidia, kuweza kurudi na kuweza kuwa katika hali yenu ya kawaida.
"Tiba dhidi ya dawa za kulevya ipo, msione aibu njooni japokuwa kuna ile hali ya kujiona kuna unyanyapaa.Lakini, sasa hivi jamii inaelewa njooni msiogope tuko pamoja kusaidiana, vita hii si ya mtu mmoja.
"Tuko pamoja tunashirikiana kusaidiana, Serikali inatoa pesa na kwa namna hiyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kwa namna moja ama nyingine toka ameingia madarakani amewekeza kiasi kikubwa cha pesa."
Pia, amesema Mheshimiwa Rais amekuwa akiwatia moyo dhidi ya mapambano ya dawa za kulevya.
Kwa hiyo, amesema jambo ambalo wanalifanya ni kuendelea kuunga mkono jitihada za Awamu ya Sita za kuhakikisha Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana.
"Ukiangalia kauli mbiu ya mwaka huu ni kumwezesha mwanamke na msichana kufikia haki yake, kufikia masuala ya usawa na pia kuwatia moyo.
"Hilo tumelifanya kwa kupitia huduma ambayo tunaitoa."
Katika ziara hiyo, wanawake kutoka DCEA wamewapatia zawadi mbalimbali wanawake wenzao ambazo zinabeba utu wa mwanamke kuonesha kuwa wapo pamoja na wanajaliana.
Vilevile ametoa wito kwa wanawake ambao wapo nyumbani huku wakiwa waraibu wa dawa za kulevya kujitokeza ili kupata huduma za methadone ili kurejesha matumaini yao upya.
Mraibu
Victoria Philipo Memba ambaye ni miongoni mwa waraibu amesema, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa huduma za Methadone ambazo zinatolewa na MAT Clinic Temeke.
"Huduma hizi zimetusaidia sana, kwa sasa ni tofauti kabisa na tulipokuja mwanzo hapa, tuko tofauti.
"Kwanza sasa hivi tunajielewa, familia inatujali, sasa hivi kila tubapokwenda watu wanatukumbuka sasa hivi, hata mtu akikuona unatembea mtaani anapenda akuone aongee na wewe."
Amesema, kutokana na thamani hiyo ambayo wameanza kupewa na jamii wanaishukuru Serikali kwa huduma hiyo ya Methadone.
Pia, amesema kupitia huduma hiyo wamekuwa wakipewa elimu kuhusu namna ya kutumia vipaji vyao ili kushiriki katika shughuli za uzalishaji katika hamii kujiletea maendeleo.
"Tunawaomba wale ambao hawajawahi kutumia dawa za kulevya wasitumie dawa za kulevya, dawa za kulevya siyo nzuri na kama kuna watu ambao wako mitaani dada, kama bado wanajifichaficha tunawaomba waje kunywa Methadone.
"Methadone inawezekana, Methadone inaponyesha na ni tiba mbadala miaka miwili mpaka mitatu."
Mraibu huyo ameishukuru DCEA kwa kuonesha upendo kwao kwani sasa wameona nuru mpya maishani mwao.
Awali, amesema alikuwa hana mwelekeo wa maisha kutokana dawa za kulevya kuharibu ndoto zake na afya.
Mathalani, kwa sasa amesema ana uhakika wa kipato na pia malazi yake yana ubora tofauti na miaka kadhaa iliyopita.
"Kwa hiyo ninashukuru kwa sasa kwa sehemu ninajiweza, hata ukienda kuomba kitu au kukopa watu wanakuwa na imani nawe tofauti na huko nyuma."
Daktari
Kwa upande wake Frida Thobias Mtui ambaye ni daktari wa magonjwa na afya ya akili katika Kituo cha Methadone Temeke amesma kuwa, kituo hicho kimeanzishwa miaka 11 iliyopita.
Ndani ya miaka hiyo, Dkt.Mtui amesema wameendelea kutoa huduma ambapo zaidi ya waraibu 3,500 wamehudumiwa.
"Kwa sasa hivi wagonjwa ambao wanapata huduma ni kama ni zaidi ya 900 ambao katika hao asilimia 3 ni wanawake."
Ukiachana na huduma za Methadone amesema, pia huwa wanatoa huduma za upimaji ws magonjwa ya VVU, homa ya ini.
Amesema, wale ambao wanagundulika wana VVU wamekuwa wakipewa huduma za ARVs, matibabu ya kifua kikuu na wenye homa ya ini huwa wanapelekwa vituo husika.
Pia, wamekuwa wakiwapa ushauri nasihi kuhusu kuacha matumizi ya dawa za kulevya na vilevi vingine.
"Na tumekuwa tukiwapa huduma ya kuwakutanisha na familia kwa kuita vikao kwa ajili ya kuja kuendelea kuwaunga mkono na kuwarudisha ili waweze kuungwa mkono na jamii."
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Siku ya Wanawake Duniani