DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezungumza hayo wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yaliyofanyika tarehe 13 Machi, 2025 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Watumishi umuhimu wa utoaji wa huduma za ushauri wa kisheria, ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo imetolewa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Tunatakiwa kuendelea kuzingatia Sheria na Kanuni tulizojiwekea ili tuweze kutoa huduma bora na stahiki kwa wananchi,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mhe. Johari amewahimiza Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kusoma Mpango Kazi wa Ofisi ili kuwianisha Mipango na Programu mbalimbali za Maendeleo ya Taifa ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoelekea kuisha na kuangalia namna bora ya kutekeleza malengo yaliyoainishwa katika Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuwahudumia wadau wote wanaohitaji huduma katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia misingi ya taaluma ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kujenga taswira nzuri ya Ofisi.

"Niwaombe washiriki wa Mafunzo haya kufuatilia kwa umakini masuala mbalimbali mtakayoelezwa na wakufunzi wetu na naamini baada ya kupata mafunzo haya utendaji kazi wetu utaenda kuwa bora zaidi,”amsema Bw. Njole.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi Faith Minani amesema kuwa mafunzo elekezi kwa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mahususi kwa ajili ya kuwajengea uwezo na uelewa Watumishi hao juu ya masuala mbalimbali ya Utumishi wa Umma ambayo yatawasaida wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Mafunzo haya maalumu yatawasaidia Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuenenda vizuri katika Utumishi wa Umma na kutoa huduma bora.”
Naye, Wakili wa Serikali Paul Mwashitete amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia aliushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaida katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.
Tags
Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Habari
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali