Watumishi wa Mahakama Dar washerehekea Siku ya Wanawake Duniani kivingine

NA BAKARI MTAULLAH

KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika Machi 8 kila mwaka, Watumishi na Viongozi Wanawake wa Mahakama ya Tanzania katika Mkoa Dar es Salaam wameungana na Watanzania wengine kusherekea maadhimisho hayo katika matukio ya aina tofauti.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, akisalimiana na mmoja wa Wanafunzi hao. Picha chini akiongea na Wanafunzi hao kwa niaba ya Viongozi na Watumishi Wanawake wa Mahakama walioshiriki katika maadhimisho hayo.
Watumishi na Viongozi hao, kwa pamoja walikusanyika katika ukumbi wa PSSSF kwenye jengo la Golden Jubilee Posta tarehe 7 Machi, 2025 kusherekea Siku hiyo iliyopambwa kwa Kauli Mbiu isemayo, “Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.”

Katika sherehe hiyo, washiriki pia walipata elimu jinsi ya utoaji haki na namna ya kuhakikisha kama kuna usawa katika jinsia zote mbili. Elimu ya uwezeshaji kiuchumi na kitaaluma pia ilitolewa katika sherehe hiyo.
Viongozi na Watumishi Wanawake wa Mahakama Mkoa wa Dar es Salaam wakifurahia kwa pamoja na Wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Sekondari Pugu baada ya kuwatembelea kama sehemu ya kusherekea Siku ya Wanawake Duniani.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu akizungumza na Wanafunzi hao baada ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwa niaba ya Viongozi na Watumishi Wanawake wa Makakama katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania katika Mkoa wa Dar es Salaam wakikata keki katika sherehe ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Picha chini, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza wakati wa sherehe hiyo.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, alieleza kuwa haki inabadilika kulingana na nyakati, hivyo kila wakati wanatakiwa kukumbushana haki hizo kwa mtazamo wa wakati husika.

Sherehe hizo zilitamatishwa tarehe 8 Machi, 2025 kwa kutembelea Shule ya Sekondari Pugu iliyopo Wilaya Ilala, ambapo Watumishi hao, wakiongozwa na Mhe. Dkt. Opiyo waliwapa faraja Wanafunzi wenye uhitaji maalum na kuwapatia zawadi mbalimbali.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, akitoa neno la ukaribisho kwa Watumishi hao, alielezea historia fupi ya shule hiyo na pia changamoto zinazowakabili watoto hao kwa sasa. 

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wazazi kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum kwa kuhisi kuwa wana mkosi.

"Watoto hawa wana uwezo mkubwa sana kielimu kiasi cha kwamba wana muda mrefu hawajawahi kupata Daraja la Nne," alisema.
Mkuu wa Msafara aliwapongea Walimu hao kwa hatua hiyo na kuwasihi wawe na moyo huo wa kuwalea vijana hao, kwa kuwa nao licha ya kuwa ni Walimu lakini pia ni Wazazi.

“Sisi katika kusherekea Siku ya Wanawake Duniani hatuna ubaguzi, hatuangalii Wanawake tu, tunaangalia pia wenye uhitaji kuliko jinsia au jinsi,"alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news