MWANZA-Mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga) wameendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuichapa Pamba Jiji FC mabao 3-0.
Ushindi wa Yanga SC katika Dimba la CCM Kirumba jijini humo haukuwa tishio kwa Pamba Jiji FC tu, bali umeongeza hofu kwa watani zao Simba SC ambao awali walikaa kileleni hapo kwa muda mrefu.
Katika mtanange huo wa Februari 28,2025 mabao ya Yanga SC yamepachikwa na Shadrack Isaka Boka dakika ya 28 kwa mpira wa adhabu.
Aidha, bwana harusi Stephanie Aziz Ki alipachika mabao mawili ndani ya dakika ya 75 na 76 na kufikisha jumla ya mabao 7 katika msimamo wa Ligi.
Kabla ya mtanange huo, Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ilikuwa imepigwa michezo miwili ya mzunguko wa 22 kwa kuchezwa viwanja viwili jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa kwanza JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya KenGold kutoka Mbeya katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam.
Mchezo ulianza kwa kasi ambapo kila mchezaji alipambana kuhakikisha timu yake inapata alama muhimu ,dakika ya 45 mchezaji wa JKT, Edward Songo aliipatia timu yake goli kwa mkwaju wa penati hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili kilianza ambapo Ken Gold walionekana wakilisaka kwa kasi lango la JKT Tanzania na dakika ya 85 mchezaji wa wao Selemani Bwenzi aliwaamsha mashabiki wa ‘makarasha’ kwa kuipatia timu yake bao la kusawazisha na kufanya mchezo kuisha wakiwa wamegawana alama moja moja.
Mchezaji wa Ken Gold Seleman Bwenzi alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.
JKT Tanzania wamefikisha alama 27 wakiwa wamefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 16 na wakiwa nafasi ya sita baada ya kucheza mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC 2024/2025.
KenGold wanaendelea kusalia nafasi ya 16 kwenye msimamo wakiwa na alama 15 wakifunga mabao 18 kuruhusu 38 baada ya mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo wa pili ni timu ya Azam iliwapokaribisha timu ya Namungo katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi.
Ilimchukua dakika 12 mchezaji wa Namungo, Hamis Halifa kuwaweka mbele timu yake kabla ya mchezaji wa Azam, Gibril Sillah kuweka mzani sawa katika dakika ya 43 ya mchezo huo hivyo timu zote kwenda mapumziko ubao ukisomeka 1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa mchezo.
Mlinda mlango wa Namungo, Jonathan Nahimana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.
Azam wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na alama 45 wakifunga mabao 32 kufungwa 12 huku Namungo wakiwa nafasi ya 12 wakiwa na alama 23 wakifunga mabao 16 na kuruhusu mabao 27.
Wakati huo huo, Yanga SC ipo kileleni ikiwa na alama 58 baada ya mechi 22 huku watani zao Simba SC wakiwa nafasi ya pili kwa alama 51 baada ya mechi 20.