ZANZIBAR-Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC),Sultan Said Suleiman amewataka washauri elekezi wa mradi wa nyumba za kisasa Chumbuni kutoka Kampuni ya Mecon kuhakikisha kazi ya kupitia upya michoro ya nyumba hizo haiathiri bei na muonekano wake.
Akizungumza katika kikao cha kubadilishana mawazo kati ya wataalamu wa kampuni hiyo na wahandisi wa Shirika la Nyumba kuhusu mapendekezo ya kuboresha michoro ya mradi huo huko katika ofisi za ZHC Darajani,Sultan amesema kazi hiyo ni muhimu.
Ni ili kuzifanya nyumba hizo ziweze kuzingatia utamaduni wa Wazanzibari, mazingira pamoja na kuwa na maeneo ya shughuli za kijamii na biashara.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu amesisitiza kuwa mabadiliko yoyote yanayopendekezwa na kuthibitishwa yasiathiri gharama za mradi na mauzo ya nyumba hizo au kwenda kinyume na mkataba wa mradi huo.
Mshauri Elekezi wa mradi wa Chumbuni kutoka Kampuni ya Mekon, Mhandisi Moses Kony amesema kuwa, mabadiliko hayo yanalenga kuongeza ubora wa mazingira ya nyumba hizo na kuahidi kuwa hayataathiri makadirio ya gharama za ujenzi au bei za nyumba hizo.
Jumla nyumba 3,000 zinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo la Chumbuni ambapo katika awamu ya kwanza nyumba 1,095 tayari zimeanza kujengwa.