Zijue faida za vituo vya ubunifu katika TEHAMA

■Vijana waitwa kuchangamkia fursa,kupewa ofisi na huduma bure miezi nane

■Dkt.Mwasaga asema hata mbunifu akiwa hana elimu milango ipo wazi

■Dhamira ni kuifanya Tanzania kuwa shindani duniani kwa bunifu, fursa za ajira

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Dkt.Nkundwe Mwasaga amesema kuwa,vituo vya ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini vipo kwa ajili ya mbunifu yeyote bila kujali ana elimu au hana elimu.
"Tunachoangalia hapa ni ubunifu, huo ubunifu tunaukuza kwa miezi nane, kwa hiyo mbunifu atapata ofisi bure, atapata mafunzo bure, atakutanishwa na mabenki, atakutanishwa na wanasheria na atakutanishwa na kila hali ambayo itamfanya yeye kuwa kampuni."

Dkt.Mwasaga ameyasema hayo Machi 16,2025 makao makuu ya tume yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kufanya ziara.

Amesema, katika kipindi hicho mbunifu atatumia rasilimali za kituo bure kama mtu akianzisha kampuni yoyote ambayo anaifungulia ofisi huko mtaani.

Ameeleza kuwa, Serikali imeanzisha vituo hivyo ili kuwaondolea vizuizi ambavyo wabunifu walikuwa wanakumbana navyo, hivyo kuwakatisha tamaa ya kusonga mbele.

"Na katika kipindi hicho atatumia rasilimali zilizopo kwenye kituo kufanya shughuli zake kama mtu akianzisha kampuni yoyote ambayo anaifungulia ofisi huko mtaani."

Amesema,kati ya vituo hivyo kuna vituo vya kukuza bunifu za vijana na vingine kwa ajili ya kutengeneza bidhaa.

Katika vituo vya kutengeneza bidhaa, Dkt.Mwasaga amesema, kimoja kipo TIRDO na kingine SIDO jijini Arusha.

Pia, amesema kwa upande wa makao makuu ya Tume ya TEHAMA jijini Dar es Salaam kuna vituo viwili.

Kati ya vituo hivyo, Dkt.Mwasaga amesema kimoja ni kwa ajili ya kukuza bunifu za vijana na kuna kituo kingine ambacho ni kati ya vituo 17 vya Umoja wa Mawasiliano Duniani.

Aidha, amesema kituo kingine kipo mkoani Lindi, Zanzibar, Tanga, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha viwili na Dar es Salaam vitatu vyote vikiwa ni kwa ajili ya vijana.

"Kwa sababu, Tanzania sisi tumepata bahati ya kuwa na vijana wengi."

Dkt.Mwasaga anasema, idadi ya vijana kwa mujibu wa Sensa ambao ni kuanzia miaka 15 hadi 34 wapo milioni 21.

"Sasa hiyo idadi ni fursa kwetu, kwa hiyo hawa vijana wanatakiwa kupata uwezo wa kuweza kubuni uanzishaji wa kampuni na hizo kampuni ziweze kufanya mambo mawili makubwa.

"Kutengeneza kazi kwa vijana wenzao na kufanya Sekta ya TEHAMA itoe mchango mkubwa katika pato la Taifa la Tanzania."

Dkt.Mwasaga amesema,jambo ambalo Serikali ililiona na ikaipelekea kuanzisha hivi vituo, ni kwamba zamani ilikuwa mbunifu akitaka kukuza ubunifu wake, kuanzisha kampuni atatakiwa lazima apate ofisi alipe kwa miezi sita au mwaka ambayo mara nyingi ilikuwa ni kizuizi kinachofanya watu wasiweze kukuza bunifu zao.

"Kwa hiyo hayo yote tumeyaangalia, vituo hivi vitakuwa si ofisi peke yake, vitakuwa na vifaa, vina wataalamu, vina mafunzo na vina fursa mbalimbali ambazo tutawapa.

"Yote haya ni katika kufanya vijana wetu waweze kufanya Tanzania iwe shindani, kikanda, kibara na kiduniani.

"Sisi kama tume kazi yetu kubwa ni kukuza, Tume ya TEHAMA siyo mdhibiti, sisi hatudhibiti, sisi kazi yetu ni kukuza hizi bunifu ziwe kampuni na ikiwezekana ziwe kampuni nyingi."

Dkt.Mwasaga anasema, kwa kufanya hivyo, Serikali ina uhakika idadi ya wabunifu nchini itaongezeka na watatengeneza kazi nyingi hata nje ya Tanzania.

Pia, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa uchumi wa kidijitali ambao ulizinduliwa mwaka jana ambao ni wa miaka 10.

"Mafanikio tuliyopata mpaka sasa hivi ni makubwa, ukiangalia katika ubunifu kwa ubora Afrika, sisi Tanzania tupo katika nchi 10."

Tukiangalia viashiria vingine kwa upande wa TEHAMA, Dkt.Mwasaga anasema kwa upande wa usalama kidunia, Tanzania inashika namba moja.

"Chama cha ITU kilifanya utafiti au thamini kimetuweka katika kundi hilo ambalo zipo nchi 34 na sisi tuko hapo."

Kwa upande wa masuala ya kupeleka Fiber katika nyumba za watu, Dkt.Mwasaga anasema, Tanzania ipo katika nchi 20 bora duniani.

"Kwa hiyo, nchi yetu imeanza kuonyesha mafanikio makubwa ambayo ukiangalia matumizi ya huduma za simu, tunatumia kwa kiasi kikubwa hasa kwa upande wa miamala."

Amesema, jambo hilo limeweka Tanzania katika nafasi nzuri huku mkakati ukiwa ni kuwafanya vijana waweze kuwa wabunif

"Kwa sababu bila ubunifu, uchumi wa kidijitali unaweza kujikuta ukawa ni mtumiaji tu, kwa hiyo tunataka tuwe na uchumi wa kidijitali ambao ubunifu mkubwa unafanyika hapa Tanzania."

Vilevile, Dkt. Mwasaga amesema, Serikali imeona ubunifu huo haupaswi kuonekana jijini Dar es Salaam peke yake bali utokee katika mikoa mbalimbali nchini.

Amesema, kutokana na maono hayo ndiyo maana Serikali imedhamiria kujenga vituo vya kukuza bunifu za vijana kote nchini.

Lengo ni kuwezesha kujenga uchumi wa kidijitali imara na wenye ushindani katika soko la nje.

"Kwa sababu ubunifu ndiyo wenye uwezo wa kuzalisha kazi nyingi sana,na sekta tulizo nazo za kiuchumi ni nyingi. Kwa hiyo, kazi inayofanyika sasa hivi kama mlivyoona mwaka jana ni kuwezesha mifumo kuzungumza na sasa hivi tunatoa Jamii Namba."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news