ZANZIBAR-Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Machi,2025 ambapo bei hizo zimetajwa kupanda.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Kaimu Meneja Kitengo cha Uhusiano, Shara Chande Omar kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) katika ukumbi wa ZURA uliopo Maisara Mjini Unguja amesema bei hizo zitaanza kutumika Machi 9,2025.
Amesema bei ya mafuta ya Petrol na Dizel na Mafuta ya ndege kwa mwezi Machi imepanda kulinganisha na mwezi Febuari.
Akizitaja bei hizo amesema, Petrol imepanda kutoka Mwezi Febuari shilingi 2,819 hadi Machi shilingi 2,939 bei ya Dizel imepanda kutoka mwezi Febuari shilingi 2,945 hadi Machi shilingi 3,135 wakati mafuta ya ndege yamepanda kutoka mwezi Febuari shilingi 2,423 hadi Machi shilingi 2,500 wakati mafuta ya taa yatabaki na bei ileile ya shilingi 3,200 kwa mwezi Machi.
Hata hivyo amesema,ZURA inapanga bei kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta Duniani, Gharama za uingizaji wa Mafuta katika Bandari ya Tanga, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta.
Pia,gharama za usafiri, Bima na Preminium hadi Zanzibar, Kodi za Tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa Wauzaji wa Jumla na Reja Reja.
Aidha,amesema sababu za kuongezeka kwa bei za mafuta kwa mwezi Machi, 2025 ni kuongezeka kwa gharama za Mafuta katika Soko la Dunia, kuongezeka kwa gharama za uingizaji wa mafuta na kuongezeka kwa wastani wa thamani ya Dola ya Kimarekani ukilinganisha na Shilingi ya Tanzania.
Mamlaka inawahimiza wananchi kununua mafuta katika vituo halali vya kuuzia mafuta na kudai Risiti za Kielektroniki kila wanaponunua mafuta hayo ili zinapotokezea changamoto zozote wapate kusaidiwa.