Na Respice Swetu
Kasulu
Mkazi wa halmashauri ya mji wa Kasulu Wencheslaus Luyaga maarufu kwa jina la Gadafi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alisafiri kwa kutumia usafiri wa baiskeli kutoka Kasulu hadi Dodoma kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi, amefanya safari nyingine ya kutoka Kasulu mkoani Kigoma hadi Tabora mjini kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.

Akizungumzia safari hiyo, Gadafi ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Junga iliyopo halmashauri ya mji wa Kasulu amesema, maamuzi ya kuibeba ajenda hiyo, yamechagizwa na mafanikio yalipatikana katika sekta ya utalii nchini baada ya Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuuhamasisha umma na dunia kwa ujumla kuhusu fursa za utalii zilizopo nchini.
Gadafi aliyeipa safari hiyo jina la “utalii wa magharibi”, anatarajia kuikamilisha safari hiyo mwishoni mwa wiki hii akiwa amepita katika maeneo mbalimbali ya utalii na uhifadhi yaliyopo kwenye mikoa ya Tabora na Kigoma ambako pia atazungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo wa mamlaka za serikali, maeneo ya makumbusho na wanaohusika na hifadhi na utunzaji wa mazingira.
Sanjari na utalii huo, malengo mengine ya “safari ya magharibi” ni kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, kuilinda amani ya Tanzania na uzingatifu katika utunzaji wa afya kwa makundi mbalimbali hususan watoto, kina mama na watu wenye ulemavu.
Katika siku za karibuni, Gadafi amepata umaarufu mkubwa kutokana na kutumia usafiri wa baiskeli kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi akiwa amebeba bendera ya mji wa Kasulu na ajenda za kitaifa.