Askofu Dkt.Shoo atoa neno kuelekea Uchaguzi Mkuu

KILIMANJARO-Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt.Frederick Shoo amewataka wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 kuhakikisha wanasimamia vizuri ili uwe huru na haki.
Pia,amewataka wasikilize sauti za wananchi, viongozi wa dini pamoja na wadau wengine wanaoitakia mema Tanzania ili uchaguzi usifanane na chaguzi zilizopita.

Dkt.Shoo ameyasema hayo Aprili 20,2025 wakati akitoa salamu za ujumbe wa Pasaka katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi Mjini, Askofu Shoo.

“Mungu ametupa nchi nzuri sana Tanzania, tuipende nchi yetu, kila mmoja ajitoe kuona Tanzania yetu imekuwa mahali salama, na kuwa mahali ambapo kila mtu atakaa kwa kufurahia na kujivunia kwamba tuna nchi nzuri, tuwe na hofu ya Mungu katika maamuzi na matendo yetu.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi tuna wajibu wa kuchagua viongozi, na ni haki yetu kupata viongozi ambao watatupeleka mbele kama nchi.

"Hivyo kama ambavyo viongozi wa dini tumetoa wito Watanzania kushiriki uchaguzi, tumetoa wito kwamba haki na wajibu huu wa raia kuchagua viongozi wanaowataka isiiingiliwe na mamlaka yoyote.

“Tunaomba sana uchaguzi huu usifanane na chaguzi nyingine zilizopita, ule wa 2019, 2020 na huu uliofanyika mwaka jana (2024), hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi nilizozitaja yakijirudia.

"Tunaomba wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi huu, sikilizeni sauti za wananchi, sikilizeni sauti za viongozi wa dini na wadau wengine wanaoitakia nchi hii mema.

“Msizibe masikio, pia nawaomba kwa kuheshimu sana jeshi letu la polisi,polisi tunawapenda sana na tunawategemea sana kwa jambo la ulinzi.

"Niwaombe katika uchaguzi huu msikubali kutumiwa kwa maslahi ya watu ambao hawaitakii nchi mema, mlitutaka tutoe ushauri, tutoe maoni, tumetoa maoni, heshimuni maoni ya Watanzania, tutaendelea kusema na mwenye kusikia asikie,"amesisitiza Askofu Dkt.Shoo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news