MBEYA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha semina maalum kwa watu wasiosikia (viziwi) kuhusu elimu ya mikopo, uwekezaji katika dhamana za serikali, pamoja na utambuzi wa alama za usalama na utunzaji sahihi wa noti.
Semina hiyo, iliyoratibiwa na Tawi la Benki Kuu Mbeya, iliwapa washiriki fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu alama za usalama zilizopo kwenye noti za Tanzania, pamoja na mbinu bora za utunzaji wa noti ili kuzuia uchakavu wa haraka.
Washiriki walielezwa kuwa uchakavu wa noti huongeza gharama ya uchapishaji wa noti mpya, hivyo ni muhimu kutunza noti vizuri ili kusaidia kupunguza gharama hizo.
Aidha, washiriki walihimizwa kuchukua mikopo kwa malengo mahsusi yanayoweza kuwaendeleza kiuchumi na kuepuka kukopa kutoka taasisi ambazo hazina leseni ya Benki Kuu. 

Vilevile walikumbushwa kuwa na tabia ya kurejesha mikopo kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na ucheleweshaji wa malipo.