NA BENNY MWAIPAJA
Washington D.C
BENKI ya Dunia imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi wa nchi na kuwa nchi ya kupigiwa mfano barani Afrika licha ya misukosuko mbalimbali ya kiuchumi inayoikabili dunia.

Dkt. Diop alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na mizozo ya kisiasa inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Aidha, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi itakayochochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimweleza Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, aliyechukua nafasi ya Bi. Victoria Kwakwa, aliyemaliza muda wake, kwamba Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania.
Alisema kuwa, usimamizi mzuri wa uchumi unatokana na mwongozo na maono makubwa ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania, ambaye ameelekeza fedha nyingi katika sekta za uzalishaji na maendeleo ya jamii lakini pia ujenzi wa miundombinu inayochochea ukuaji wa uchumi.

