DAR-Wananchi wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga wamemtaka Mbunge wao, January Makamba kujiuzulu nafasi hiyo kwani ameshindwa kutekeleza aliyowaahidi wakati wa kampeni.
Wamesema, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kura zote za Urais watampa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, lakini ubunge hawatampa January Makamba.
Wameyasema hayo leo Aprili 2,2025 jijini Dar es Salaam wakati wakizungumza na wanahabari huku wakisisitiza kuwa, miaka 15 ya Makamba imekuwa mateso jimboni humo.
"January Makamba hajafanya maendeleo tunayohitaji katika jimbo letu, sisi wana Bumbuli tunasema Makamba ajiuzulu, lakini Mama Samia mitano tena."

Miongoni mwa wananchi hao, Bw.Eric Edward kutoka Jimbo la Bumbuli katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli amesema kuwa, miongoni mwa kero ambazo waliamini Makamba angezipatia ufumbuzi ni ya barabara ili waweze kusafirisha chai kwa urahisi, lakini hadi sasa mambo yapo hovyo.
“Kero kubwa ni chai, kiwanda cha Mponde mara nyingi sana wanasema ivumayo haidumu, hiki kiwanda mara ya kwanza kilikuwa na magari mazuri, lakini kwa sasa hivi chai imeshuka thamani yake kabisa.
"Sisi ni wakulima kuja barabara ya mashamba kama Ngazi, Kileo na Lusanga , watu wanapata shida sana kipindi hiki cha mvua za masika , mtu anashuka na gunia la kilo 100, barabara yenyewe ni ya miguu, magari mabovu, chai inabebwa na bajaji, ni kitu cha kusikitisha sana lakini wapiganaji wengi waliopita akiwemo William Shelukindo na Januari Makamba kila mtu amepewa keki yake ya miaka 15.
"Hiyo keki imeisha, kwa hiyo mbio za kijiti hizi wamwaachie mwingine.”
Naye Elias Kamute ambaye ni mwananchi wa Jimbo la Bumbuli amesema kuwa,
“Bumbuli ina maji kama Edeni, lakini mpaka hivi leo tunafungua mabomba yanatoka sasa hivi ila baada ya muda hakuna maji,hivyo yamekua ya mgao, maji yetu siyo ya pampu, miaka yote tunapewa ahadi kwamba mabomba yatapita na matenki yatatengenezwa ila hakuna kinachoendelea mpaka sasa ni zaidi ya miaka 15 , na makamba bado yupo, na maji tunapata ya mgao hadi leo.
"Mpaka hapo makamba ameshindwa hili jimbo, tunaomba Makamba atukabidhi jimbo tumtafute mwingine aendelee na jimbo hili la Bumbuli.”
Kwa upande wake,Khalid Kijazi amesema kuwa,“Mimi ni kijana mkereketwa katika Jimbo la Bumbuli, Makamba hakufanya maendeleo tunayoyahitaji katika Jimbo la Bumbuli sisi Wanabumbuli tunamuona Mheshimiwa ni kama mtalii wa kwenda nchi za nje na Dar es Salaam bila kuja kuangalia changamoto za jimboni kwake, wananchi wa kule wanapata tabu sana.
"Kwa hiyo huyu ni mtalii na siyo mbunge wa jimbo la Bumbuli, tunaomba aachie ngazi, tuchague uongozi mwingine hatumuhitaji tena."
Mwananchi mwingine wa Bumbuli, Ayubu Radhid amesema kuwa,"Jimbo la Bumbuli lilikuwa ni tegemezi kwa wilaya kwa ajili ya kuwalisha wakazi wa Wilaya ya Lushoto,lakini baada ya miundombinu kuharibika ya barabara watu wanalaamika mpaka sasa hivi mazao yao yanaharibika kwa kukosa usafiri, hivyo Mama mitano tena, Januari ameshindwa kutuwakilisha inavyostahili.”
Wakati huo huo, mwananchi mwingine Merry Gendo amesema kuwa,
“Kero yangu mimi ni kwa ajili ya asilimia 10, tuliahidiwa tujiunge vikundi ili tuweze kuwezeshwa wajasiriamali wadogo wadogo,lakini tumeunda vikundi na hatujawezeshwa mpaka leo na kero nyingine ni maneno ya kashfa kutoka kwa Mheshimiwa January Makamba.
...siku moja alisimama akasema sisi wana Bumbuli hatuhitaji maendeleo bali tunahitaji fedha ya dagaa tu, na siku nyigine alisema Bumbuli ni jimbo lake amelinunua na fedha yake.
"Mwalimu Julius Nyerere alisema uongozi wa kununua haufai, na sisi tunasema January hatufai maana anasema amenunua Jimbo la Bumbuli.
"Jimbo la Bumbuli siyo mali yake, akapumzike na aingie mwingine atakayetuongoza kwa haki.”
Naye Iddy Amiri amesema, “Kwa upande wa Afya, Bumbuli watu wanateseka na wanakufa, tuna ukosefu wa madaktari na madawa, lakini Mheshimiwa Makamba ameshindwa kuliangalia hili na aliliahidi kwa miaka mingi, lakini alishindwa kulitekeleza mpaka leo hii.
