CCM yadumisha mahusiano imara na Vyombo vya Habari, CHADEMA yapuuza wadau muhimu wa demokrasia

KATIKA historia ya kisiasa ya Tanzania, uhusiano kati ya vyombo vya habari na vyama vya siasa umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza demokrasia, kuelimisha umma, na kushajihisha uwajibikaji wa viongozi.
Hata hivyo, tofauti kubwa imeanza kujitokeza kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA kuhusu namna wanavyoyathamini na kushirikiana na vyombo vya habari.

Kwa upande wa CCM, historia inaonyesha kuwa chama hiki kimekuwa bega kwa bega na wanahabari kwa muda mrefu.

Kutoka kwenye vikao vikuu vya chama, mikutano ya kisiasa hadi utekelezaji wa sera serikalini, CCM imehakikisha kuwa wanahabari wanapata taarifa kwa wakati, wanahusishwa kwenye matukio, na wanaheshimiwa kama sehemu muhimu ya mfumo wa utawala bora.

Hii ndiyo sababu waandishi wengi nchini wanaona CCM kama chama kinachojali mazingira ya kazi ya vyombo vya habari.

Kwa upande mwingine, wapo waliowahi kufanya kazi ndani ya CHADEMA na wameeleza wazi namna chama hicho kinavyoshindwa kuthamini mchango wa waandishi. 

Mmoja wao ambaye aliwahi kushiriki operesheni mbalimbali za chama hicho anasimulia:

“Mimi nimefanyakazi na CHADEMA. Nimesafiri sana nao kwenye kampeni mbalimbali hasa operesheni Sangara. Waandishi wa habari kwao siyo kipaumbele kabisa. Treatment yao kwa media ni tofauti sana na CCM.”

Kwa mujibu wa simulizi hiyo, hata posho za waandishi zilihitaji mtu ‘kuwa chawa’ au ‘kubembeleza’ ndipo alipata haki yake ya msingi.

Hakukuwa na mfumo wa kimaadili wala wa kitaasisi wa kushughulika na waandishi wa habari waliokuwa wakitoa jasho lao kuhabarisha jamii.

“Nilipanda Mohamed Trans kurudi Dar bila kumwambia mtu yeyote, hata bosi wangu alishtuka kuniona ofisini. Nilimwambia sitaki tena kusafiri na hawa wahuni...”

Kauli hizi ni ushahidi wa namna baadhi ya viongozi wa CHADEMA walivyoshindwa kutengeneza mazingira rafiki kwa waandishi wa habari waliokuwa nao bega kwa bega wakati wa harakati za kisiasa.

Mbaya zaidi, licha ya mchango mkubwa wa vyombo vya habari hadi kufanikisha Chadema kuingiza zaidi ya wabunge 90 mwaka 2010, chama hicho hakijawahi kutoa hata tangazo la robo ukurasa kwenye magazeti-licha ya ruzuku ya mabilioni walizopokea.

Vyombo vya habari vilivyowawezesha sasa vinaonekana kupuuzwa, kudharauliwa, au kutakiwa vitembee na Chadema bure.

“Vyombo vya habari havifanyi kazi kwa hisani. Vinafanya biashara, kwa hiyo vinaangalia kunakolipa.”

“CHADEMA imeshawahi kufanya nini kusaidia vyombo vya habari kustawi? Hata Tanzania Daima, gazeti lao, limewashinda kuliendesha.”

Katika mazingira haya, ni wazi kuwa CHADEMA haioni umuhimu wa kuwa na kanzidata (database) ya waandishi wa habari mikoani, kuwahusisha kwa kupiga simu, kuwapa taarifa au hata kufuatilia coverage ya mikutano yao.

Mwandishi yuko Mbeya Mjini, mkutano unafanyika Mbozi hawamsafirishi, hawampatii posho, halafu wanalalamika asipoandika habari?.

Huu ni uthibitisho kwamba tofauti kati ya CCM na CHADEMA si tu kisera, bali pia ni kiutendaji na kimahusiano.

CCM inatambua kuwa waandishi wa habari ni mhimili muhimu wa utawala wa sheria, uwazi, na maendeleo. CHADEMA, kwa upande mwingine, inaonekana kutaka kurudi nyuma kifikra, ikiishi kwenye taswira ya "tunapendwa bila kufanya kazi ya kushirikiana."

Katika ulimwengu wa kisasa wa mawasiliano, vyombo vya habari siyo mapambo ya kisiasa bali ni daraja la mawasiliano kati ya viongozi na wananchi. 

Chama chochote kinachopuuza vyombo hivi ni kama kinakata matawi ya mti unaokilinda dhidi ya upepo mkali wa kisiasa.

CCM imebaki kuwa tegemeo la waandishi. CHADEMA bado wanahitaji kujifunza kuheshimu, kushirikiana na kulinda maslahi ya tasnia ya habari kama njia ya kuijenga demokrasia yenye mashiko na usawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news