NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imesema, hakuna kiongozi au mtumishi wa umma atakayesalimika kwa kuhusika kufanya uzembe hadi dawa za kulevya zikaingizwa nchini.
DCEA imesema viongozi wa vitongoji,vijiji na kata nao watahusishwa na kadhia hiyo kwa vile wanafumbia macho uhalifu unapofanyika katika maeneo yao kutokana kuwepo kwa mashamba makubwa ya bangi ambayo yanalimwa na viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa Aprili 24,2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu operesheni iliyofanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ambayo ilifanikisha kukamata wahalifu na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya.
Amesema, katika oparesheni hizo zilizofanyika mikoa saba ikiwemo Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha walifanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria nchini.
Lengo la kemikali hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kutengeneza dawa za kulevya, pia walikamata kilogramu 4,568 za dawa za kulevya huku watu 35 wakikamatwa kutokana na operesheni hiyo ya kati ya mwezi Machi na Aprili,2025.
Vilevile walikamata pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi yenye sumu hatari ikiwa ni zaidi ya Skanka.
Amesema, pia katika operesheni hiyo walifanikiwa kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi pamoja na kushikilia magari saba, pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.
Kamisha Jenerali Lyimo alisema,Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na wahalifu wa dawa za kulevya nchini ukilinganisha na miaka ya huko nyuma.
TAKUKURU
Mkurugenzi Msaidizi Malalamiko chini ya Idara ya Uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) amesema, Phobias Ndaro amesema, wanashirikiana na DCEA kukabiliana na magenge ya uhalifu wa dawa za kulevya, kwa vile yana uwezo mkubwa wa kifedha katika kusafirisha, kuingiza na kuuza dawa hizo nchini.
Pia,alisema DCEA imekuwa ikiteketeza mashamba makubwa na bangi na kukamata dawa hizo, lakini cha kushangaza zinapopita na kulimwa wapo watumishi wa umma, hivyo kuna viashiria vya rushwa.
Amesema,pengine wahalifu hao wanatumia fedha kuwahonga watumishi hao ili waweze kutekeleza uhalifu wao.
Alieleza kuwa, TAKUKURU na DCEA wameingia mkataba ili kukabiliana na watumishi wa umma wanaohusika kuchukua rushwa na kuruhusu dawa kuingia ndani au kulimwa katika misitu ya mikubwa ya Serikali.
Ndaro amesema, dawa za kulevya zina madhara makubwa ya kiuchumi, kiusalama na kijamii, hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao wataobainika kujihusisha na kadhia hiyo.
"Kwa vyovyote vile magenge ya uhalifu yanatumia fedha katika kufanikisha mazoezi ya uhalifu, tumeona hapa kuna usafirishaji, uingizaji na uuzaji.
"Hayo yote yanafanikiwa kwa sababu ya nguvu ya fedha, wanapita kwenye mipaka, wanapita sehemu mbalimbali nchini, mashamba ameeleza hapa Kamishna Jenerali yamekamatwa hii yote inaashiria kwamba kuna viashiria vya rushwa."
Ndaro kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambaye alimwakilisha katika mkutano huo na wanahabari amesema kuwa, pamoja na jukumu lao la uelimishaji umma ambalo wameingia mkataba na DCEA bado wana jukumu lao la msingi la kupambana na rushwa.
"Na kwa sababu hapa kumekuwa na viashiria vya rushwa, kwa hiyo ni jukumu letu kuhakikisha yale yote yaliyosemwa na Kamishna Jenerali (DCEA) kuhusiana na watumishi wote ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine kama watumishi wa umma tutahakikisha kwamba tunawafuatilia."
SOMA Ushirikiano wa DCEA na TAKUKURU
Amesema,dawa za kulevya kama alivyosema Kamishna Jenerali Aretas Lyimo zina madhara makubwa kwa jamii.
Kwani,pia ni chanzo cha kudhoofisha afya za vijana na kuongeza mmomonyoko wa maadili katika jamii ikiwemo ongezeko la uhalifu na wizi.
"Lakini, pia dawa za kulevya zina madhara kiuchumi, utakatishaji wa fedha kama alivyosema Kamishna Jenerali (DCEA) ambapo fedha chafu zinaweza kuingizwa kwenye mzunguko."
Amesema, wakati mwingine unaweza kukuta hata uwekezaji unafanyika kwa fedha chafu ambapo wanaojihusisha na uhalifu huo wanaweza kutumia fedha kununua vipande katika mifuko ya uwekezaji.
Pia, amesema magenge ya uhalifu wa dawa za kulevya huwa na tabia ya kupanga Serikali wanayoitaka, kufadhili makundi ya kigaidi na uhalifu mwingine.
"Wanafadhili makundi mbalimbali kwa malengo yao ili waweze kufanikisha kuendelea kufanya hiyo biashara.
"Kwa hiyo, nitoe tahadhari kama alivyosema Kamishna Jenerali (DCEA), Mkurugenzi Mkuu (TAKUKURU) ameniagiza nitoe onyo kwamba wale wote ambao wanajihusisha na hii biashara ambayo ni biashara hatari kama ambavyo nimebainisha kiuchumi, kiusalama na kijamii watachukuliwa hatua.
"Na uchunguzi unaendelea kadri tunavyopokea taarifa kwa sababu tuna mkataba wa ushirikiano tunashirikishana taarifa, kwa hiyo uchunguzi unaendelea kwenye maeneo yote hayo.
"Kwa hiyo Mkurugenzi Mkuu anatoa onyo kwa watumishi wote wa umma, wawe waadilifu na watangulize uzalendo katika kutekeleza majukumu yao.
"Haiwezekani watumishi wa umma wapo kwenye hayo maeneo hayo, lakini dawa za kulevya zinapita na zinaingizwa, haiwezekani.
"Na wale wote ambao uchunguzi utabainisha kwamba wamejihusisha hatua kali zitachukuliwa kama alivyosema Kamishna Jenerali (DCEA), kwa upande wetu (TAKUKURU) kama amejihusisha tutataifisha mpaka mali zake ili jamii yetu ione kwamba hii ni biashara haramu na ni vita."
Pia, ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuelimisha jamii ili iweze kutoa taarifa kuhusu matukio ya dawa za kulevya na viashiria vya rushwa.
Kwani, kama biashara hiyo inavyofanywa kwa siri, jamii nayo inapaswa kutoa taarifa za siri ili mamlaka hizo ziweze kuchukua hatua za haraka na jamii iweze kubaki salama bila dawa za kulevya na vitendo vya rushwa nchini.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Programu Rafiki ya TAKUKURU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)