📌 Azindua Shule ya Sekondari Migungani, awataka wanafunzi kutunza miundombinu
📌 Asema Serikali yajipanga kujenga mradi mkubwa wa umeme Monduli
ARUSHA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa jitihada zao za kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.

“Naomba kuwapongeza tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Monduli.
"Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.

Akiwa shuleni hapo, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi kwa kujenga shule hiyo ya Sekondari Migungani na kufikia asilimia 85 ya ujenzi huku Serikali ikichangia shilingi milioni 500.
“Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo. Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni miongoni mwa shule zilizopo Wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu kwa vijana wetu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na wananfunzi 400 na hivyo amewataka wanafunzi kutunza miundombinu sambamba na kujifunza kwa bidi ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema huku wakiwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.
Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kwa lengo la kuuongezea nguvu umeme unaopatikana ili uweze kufika Loliondo na kusaidia wilaya hiyo kuwa na umeme wa uhakika.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema kuwa Wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi na wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.