WASHINGTON-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kampuni ya VISA anayesimamia Ukanda wa Ulaya ya Kati, Mashariki ya Kati na Afrika, Bw. Andrew Torre.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili kwa kina namna mbalimbali za kupunguza gharama za miamala ya kifedha, kudhibiti uhalifu wa kimtandao, na kuimarisha utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi.
Masuala hayo yanalenga kupunguza matumizi ya fedha taslimu pamoja na kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma rasmi za kifedha, hasa zile zinazotolewa kwa njia ya kidigitali.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Missango, Meneja wa Sera ya Fedha BoT, Bi. Asimwe Bashagi, pamoja na maafisa waandamizi kutoka kampuni ya VISA.
