ARUSHA-Washiriki wa Jukwaa la Nne la Usalama Mtandaoni (The 4th Tanzania Cybersecurity Forum 2025) wameazimia mambo 14 ambayo wanaamini yataleta matokeo chanya katika usalama mtandaoni nchini.
Maazimio hayo wameyafikia leo Aprili 11,2025 katika hitimisho la siku mbili za kusanyiko la wanajukwaa hao ambalo lilianza Aprili 10,2025 katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.
Jukwaa hilo muhimu limewakutanisha wadau muhimu kutoka serikalini, sekta binafsi, vyuo vikuu, asasi za kiraia na washirika wa kimataifa kwa lengo la kushirikiana, kubadilishana maarifa, na kujengeana uwezo.

Sambamba na uelewa wa kukabiliana na mabadiliko yanayosambaa kwa kasi katika mazingira ya usalama mtandaoni na matishio mbalimbali.
Pia, Dkt.Mwasaga amesema, washiriki hao pia wameazimia kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni miongoni mwa wataalamu wa usalama mtandaoni ili kuboresha usimamizi wa taarifa na usalama wake.
Jambo lingine ni kuimarisha Kituo cha Usimamizi wa Viwango vya Usalama Mtandaoni (CERT) kwa kujenga uimara katika sekta zote za uchumi kupitia ushirikiano, uelewa na uendelezaji wa uwezo wa kitaalamu.
Dkt.Mwasaga amesema, azimio lingine ni kuhamasisha upatikanaji wa taarifa kwa wavumbuzi, kuimarisha mbinu za ulinzi wa taarifa na kuanzisha huduma nafuu za kuhifadhi taarifa ndani ya nchi.
Pia kufanya ukaguzi wa matumizi ya IoT (Internet of Things) katika sekta mbalimbali ambapo Dkt.Mwasaga ametolea mfano Sekta ya Kilimo na nyinginezo.
Washiriki, pia wameazimia kukuza usawa kati ya ubunifu wa kidijitali na usalama, hasa katika kulinda watoto dhidi ya hatari za mtandaoni.
Azimio la lingine, Dkt.Mwasaga amesema, ni kufanyia mapitio mikakati ya usalama mtandaoni na ulinzi wa watoto mtandaoni ili kujenga mazingira salama na yenye uwajibikaji mtandaoni.
Vilevile, amesema wameazimia kuhamasisha uundaji wa ajira, kujenga imani ya matumizi sahihi ya huduma za kidijitali na kuimarisha imani ya wawekezaji kupitia uwekezaji katika sekta hiyo.
Dkt.Mwasaga ameongeza kuwa, washiriki kwa umoja wao wameazimia pia kutetea suluhisho za usalama mtandaoni zilizobuniwa ndani ya nchi kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi pamoja na mafunzo nafuu kwa vijana.
Lengo amesema ni ili kuwawezesha kukuza kampuni changa (startups) na kuimarisha uimara wa Tanzania katika nyanja ya kidijitali
Katika azimio lingine, Dkt.Mwasaga amesema, washiriki wameazimia kukuza ushirikiano kati ya sekta ya viwanda na elimu ili kuwapa wanafunzi uzoefu wa moja kwa moja katika sekta ya usalama mtandaoni, na hivyo kuboresha ujuzi wao na uwezo wa ubunifu katika ulinzi wa kidijitali.
Jambo lingine, wameazimia kuhamasisha matumizi ya programu tumizi (apps) zilizotengenezwa ndani ya nchi katika sekta ya umma na binafsi ili kuunga mkono ukuaji wa suluhisho za usalama mtandaoni zilizobuniwa Tanzania.
Mbali na hayo, Dkt.Mwasaga amesema, washiriki wameridhia kuunda mfumo wa kampuni changa za usalama mtandaoni unaotoa suluhisho ndani ya nchi kwa changamoto za kiuchumi za kidijitali ndani na nje ya nchi.
Azimio lingine ni kuanzisha programu ya ulezi (mentorship) kwa miradi ya wanafunzi kwa kushirikiana na viongozi wa sekta ya usalama mtandaoni.
Dkt.Mwasaga amesema, pia washiriki wameazimia kuanzisha rejista za taarifa katika sekta ya umma na binafsi ili kuimarisha uchumi wa kidijitali wa Tanzania.
Jukwaa hilo la siku mbili limeongozwa na kaulimbiu isemayo, "Kuimarisha Uimara na Kukabiliana na Vitisho Katika Uchumi wa Kidijitali".
Aidha, limejumuisha mijadala ya wataalamu, warsha za kiufundi, mijadala ya kisera, fursa za kujenga mtandao wa ushirikiano, pamoja na mafunzo ya vitendo yenye lengo la kuimarisha uimara wa Tanzania dhidi ya matishio ya usalama mtandaoni.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya mtandao endelevu na jumuishi, kuendeleza uimara wa sekta muhimu.
Mada nyingine ni namna ya kulinda mtandao katika enzi ya teknolojia zinazoibuka na nyingine ni namna ya kutumia mtandao kama injini ya ukuaji wa uchumi.
Wakati huohuo, Dkt.Mwasaga hakusita kuwaeleza washiriki namna ambavyo Tanzania ya Kidigitali ilivvyoshika kasi na kwa sasa taasisi nyingi mifumo imeanza kusomana.
Dkt.Mwasaga amewataka vijana wabunifu wa Kitanzania kuongeza bidii katika bunifu zao kwani, Taifa linawategemea katika kukuza uchumi wa Kidijitali huku akisisitiza umuhimu wa bunifu za programu tumizi kwa wingi nchini.