Kundi la fisi laacha simanzi kwa mfugaji Simiyu

SIMIYU-kundi la fisi limevamia nyumbani kwa Mageni Maduhu katika Mtaa wa Mahina uliopo Kata ya Somanda, Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu na kuua kondoo wake 21 huku wengine tisa wakiwa hawajulikani walipo.
Maduhu amesema,tukio hilo limetokea Aprili Mosi, 2025 majira ya saa nne usiku, na kushangaza wengi katika eneo hilo.

"Nilianza kusikia mlio wa fisi mmoja majira hayo ya usiku, nikatoka nje na kuanza kumkimbiza.Lakini baada ya kumkimbiza fisi huyo, nilikutana na kundi jingine la fisi ndipo nilipoamua kurudi nyumbani.

"Nilipofika kwenye zizi la kondoo, niliwakuta kondoo wangu wakiwa wamekufa na damu nyingi.

"Kwenye zizi kulikuwemo kondoo 30, ambapo 21 walishambuliwa na kufa. Kondoo wengine 9 hawapo hadi sasa, na baadhi ya kondoo walikuwa na mimba na wameuawa. Fisi walikuwa wengi sana."

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahina, Mangu Mangolyo akizungumzia tukio amesema, "Tukio hili linashangaza kwani halijawahi kusikika au kuonekana fisi wakishambulia au kula kondoo wengi kiasi hiki. Nilifika kwenye tukio na kukuta kondoo wote wakiwa wamekufa."

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, ambaye alifika kwenye eneo la tukio, alisema, "Mpaka sasa bado tunaendelea na uchunguzi kubaini kama ni kweli fisi ndiyo wametenda tukio hili au la. Vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na mamlaka ya wanyamapori, vinaendelea na uchunguzi.

"Tunatoa pole kwa familia iliyokubwa na tukio hili, na tunatangaza kuanza rasmi kwa msako wa fisi katika maeneo yote yenye vichaka kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi. Tumeanza kupata taarifa za uwepo wa fisi katika maeneo haya."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news