NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),CPA Habibu Suluo amesema,katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wamesogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa kufungua ofisi katika maeneo ya kimkakati nchini.

Lengo ni kudhibiti huduma za usafiri kwa njia ya reli, barabara na waya ikipokea majukumu hayo kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
LATRA ilianza kazi rasmi Aprili 29,2019 baada ya Sheria yake kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 358 la Aprili 26, 2019.
CPA Suluo ameyasema hayo leo Aprili 14,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha mamlaka hiyo na wahariri, waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Amesema, miongoni mwa maeneo ambayo mamlaka hiyo imesogeza huduma kwa kufungua ofisi 10 katika halmashauri za miji na wilaya.
"LATRA imefungua ofisi ndogo 10 kwenye maeneo mbalimbali ya kimkakati na hivyo kuwa na jumla ya ofisi 37 nchi nzima.
"Kufikia mwezi Machi 2025, ofisi hizi ndogo zimeonesha mafanikio katika kufikia wananchi walio mbali na miji mikuu ya mikoa,kuboresha udhibiti wa bodaboda, kutatua migogoro ya wadau katika maeneo hayo.
"Na kufikisha elimu kwa wadau,kusogeza ushirikiano na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo hayo, ikiwemo Serikali za Mitaa (LGAs), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mamlaka zingine zilizopo kwenye maeneo hayo."
Maeneo hayo, CPA Saluo amesema ni Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi, Tegeta, na Mbagala jijini Dar es Salaam.
Ameyataja maeneo mengine kuwa ni Makambako mkoani Njombe, Kahama mkoani Shinyanga, Masasi mkoani Mtwara, Ifakara mkoani Morogoro,Korogwe mkoani Tanga, Same mkoani Kilimanjaro na Nzega mkoani Tabora.
"Hatua hii ni sehemu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea na juhudi za kusogeza huduma za LATRA karibu na wananchi,taratibu za kuanzisha ofisi zingine tano zinaendelea katika maeneo ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Mkuranga mkoani Pwani, Chunya mkoani Mbeya, Mufindi mkoani Iringa na Nyakanazi mkoani Kagera.