Maeneo yote nchini kufikiwa na huduma za mawasiliano-Mhandisi Mahundi

DODOMA-Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb.) amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, pamoja na mradi mwingine wa minara 636 ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za mawasiliano katika maeneo mengi ya nchi.
Mhandisi Mahundi alitoa kauli hiyo Aprili 10, 2025, Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Esther Midimu, aliyeuliza kuhusu ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika vijiji vya mkoa wa Simiyu ambavyo bado havina huduma hiyo.

“Serikali inatekeleza ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, pamoja na mradi mwingine wa minara 636. TTCL nayo itaendelea kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali. Kukamilika kwa miradi hii kutaongeza ubora wa huduma za mawasiliano nchini,” alisema Mhandisi Mahundi.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilolo, Mhe. Justin Lazaro Nyamoga, kuhusu ujenzi wa minara ya mawasiliano katika vijiji vya Lukani na Ng’uluhe, Mhandisi Mahundi alisema kuwa Serikali, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ilifanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilolo mwaka 2021/2022 kwa lengo la kubaini maeneo yenye changamoto ya mawasiliano ya simu.

Katika tathmini hiyo, changamoto za mawasiliano zilibainika katika kata za Ibumu, Irole, Uhambingeto, Kimala, Mahenge na Masisiwe ambazo zilijumuishwa katika mradi wa ujenzi wa minara 758 unaotekelezwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, ukiwa na jumla ya kata 713 zinazofikiwa na mradi huo ambapo kata mbili za Irole na Masisiwe umekamilika, na kazi inaendelea katika kata nyingine nne.

“Kwa sasa, Wizara kupitia UCSAF ipo katika hatua za maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya kumi ya mradi wa mawasiliano vijijini, ambapo Kata ya Ng’uruhe, hususan vijiji vya Lukani na Ng’uluhe kama alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, vitaingizwa katika zabuni hiyo. Utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2025/2026,” alifafanua Mhandisi Mahundi.

International news

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post