BAADA ya wakulima wa zao la parachichi kuanza kutumia mbolea katika kilimo hicho, uzalishaji umeongezeka.

Ongezeko hilo la matumizi ya mbolea limechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa parachichi inayouzwa nje kutoka tani 17,711 mwaka 2019/2020 hadi kufikia tani 35,627 mwaka 2023/2024.

Bi. Bolle alieleza kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia TFRA za kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo.

Aidha, alibainisha kuwa TFRA imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kusajili wakulima, ili kuwa na takwimu sahihi ambazo pamoja na manufaa mengine zitawezesha kuwahudumia kwa ufanisi kulingana na mahitaji yao ya mbolea.
Mkakati mwingine muhimu ni kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Bi. Bolle, kutokana na utekelezaji wa mpango wa ruzuku, matumizi ya mbolea yameongezeka kwa kasi kutoka tani 363,599 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 840,714 katika msimu wa 2023/2024-ishara ya mafanikio makubwa ya mikakati ya Serikali katika Sekta ya Kilimo.
Vilevile, Serikali inashirikiana na viwanda vya mbolea nchini ili kufanya tafiti zitakazowezesha upatikanaji wa mbolea maalum kwa ajili ya zao la parachichi.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kati, Allan Mariki ametoa wito kwa wakulima kuendelea kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali ili waweze kupata mbolea ya ruzuku itakayowaongezea tija kwenye shughuli zao.
Amesema,mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kutumia mbolea kwenye shughuli zao pamoja na kuwahamasisha kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali wa pembejeo za kilimo ili kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali kwa wakulima.