KIGOMA-Aprili 8, 2025, Mahakama ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma imewatia hatiani Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kakonko, Mhandisi Benjamin Mjuni Brighton (37) na wenzake wawili.

Wengine waliotiwa hatiani ni Fundi Sanifu wa RUWASA Wilaya ya Kakonko,Bi. Faraja Charles Kalokola (27) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chiganda Construction Limited Bw. Johansen Martine Muganyizi (46).
Kwa pamoja walishtakiwa kwa makosa ya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri,kujipatia manufaa, ubadhirifu na ufujaji.
Vilevile,matumizi mabaya ya mamlaka pamoja na ushawishi kinyume na vifungu vya 22, 23 (1), 28 (1), 31 na 33 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura namba 329 Marejeo ya mwaka 2022 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza, kifungu cha 57(1) na kifungu 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura namba 200 Marejeo ya Mwaka 2022.
Washtakiwa wamehukumiwa kulipa faini ya sh. 4,000,000/= na kurejesha sh. 53,922,660/= zilizofanyiwa ubadhirifu.