NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)
imesema,katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imerekodi mafanikio makubwa.
Hayo yamesemwa Aprili 14,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo kwenye mkutano na wahariri na waandishi wa habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
CPA Suluo amesema, LATRA inajivunia kubuni na kukuza matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye utoaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.
Ameitaja mifumo iliyobuniwa na inayotumiwa na LATRA kuwa ni Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (Railway and Road Information Management System-RRIMS),
Pia,Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaofahamika kwa jina la Safari Tiketi, Mfumo Shirikishi wa Huduma kwa Wateja pamoja na Mfumo wa e-Mrejesho.
CPA Suluo amesema, Mfumo wa RRIMS unawezesha utoaji leseni, usajili madereva, malipo na taarifa za udhibiti uliounganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za serikali kama vile TRA, TIRA, NIDA, GePG na BRELA ili kurahisisha uhakiki wa taarifa za mteja.
Amesema, mfumo huo pia unamwezesha msafirishaji kufanya maombi ya leseni na huduma zake pamoja na kuchapa leseni iliyoidhinishwa ndani ya saa 24 bila uhitaji wa kufika ofisi za LATRA.
CPA Suluo ameongeza kuwa, hatua hiyo inapunguza kwa kiwango kikubwa usumbufu na muda wa kupata huduma.
Akizungumzia Mfumo wa VTS, CPA Suluo amesema kuwa, ni mfumo unaosimamia usalama wa huduma unaotumia satelite, Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD),
Mtandao wa Mawasiliano na Vifaa vya Uhifadhi Data Taarifa (GPS Data Servers) vinavyofanya kazi kwa pamoja ili kutuma taarifa za mwenendo wa safari za chombo husika.
Amesema,kufikia Machi 2025, jumla ya magari 11,826 yalikuwa yameunganishwa kwenye mfumo ambapo kati ya hayo, magari 8,969 yanayotuma taarifa kwenye mfumo mpaka sasa.
CPA Suluo amesema,katika magari yasiyotuma taarifa, baadhi hayapo barabarani kutokana na sababu mbalimbali kama vile matengenezo ya muda mrefu, ajali, kuungua moto na baadhi yamebadili njia na kuhamia kwenye njia ambazo hazina uhitaji wa kufunga mfumo huo.
Aidha, CPA Saluo ameutaja Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaopatikana kwenye simujanja ‘Play Store’ za aina ya Android kuwa, unamuwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi.
Pia, amesema mfumo huo unamwezesha mwananchi kutambua uhalali wa leseni za magari na adhabu, hivyo kumuwezesha abiria kuepuka kutumia gari lenye changamoto ili kujiepusha na usumbufu.
CPA Suluo amesema LATRA kwa kushirikisna na wadau wametengenza Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) au Safari Tiketi uliounganishwa na mifumo mingine ya utoaji tiketi ukiwemo wa TRC na mifumo ya tiketi za mabasi.
Lengo la kufanya hivyo, CPA Saluo amesema ni ili kurahisisha ukataji tiketi na kutunza taarifa za abiria ambapo ukikamilika utaelekezwa kwenye mabasi ya mijini maarufi daladala na usafiri wa kukodi.
Amesema,tangu kuanza kuunganisha mifumo ya Tiketi za Kielektroni kwenye CeTS, tarehe 2 Agosti,2024 hadi tarehe 31 Machi, 2025, taarifa zao zinaonesha jumla ya abiria kwa maana ya miamala ya tiketi za kielektroniki milioni 13,429,549 ilifanyika kwenye CeTS.
"Idadi hii ni sawa na wastani wa abiria (miamala) 58,137 zinaonekana kwa siku, sawa na wastani wa abiria (miamala) 1,744,100 kwa mwezi katika kipindi hicho cha siku 231, takribani miezi nane tangu kuanza kutumia mfumo huu."
CPA Suluo amesema, LATRA inapokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa kutumia Mfumo Jumuishi wa Huduma kwa Wateja ambapo mwananchi anaweza kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110019 au 0800110020.
Leseni
Wakati huo huo, CPA Suluo amesema,pia mamlaka imepiga hatia kubwa katika udhibiti wa usafiri wa barabara na utoaji leseni kwa vyombo vya usafiri kwa njia ya barabara.
CPA Suluo amesema,kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)( b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, LATRA ina wajibu wa kutoa,kuhuisha,kusitisha au kufuta leseni za usafirishaji.
Amesema,idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 (Februari, 2021) hadi 334,859 mwaka 2024/25 (Machi, 2025) ikiwa ni ongezeko la leseni 108,658, sawa na ongezeko la asilimia 48.
"Hili ongezeko ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne."
Ofisi
Pia, CPA Saluo amesema kuwa, LATRA imefungua ofisi ndogo 10 kwenye maeneo mbalimbali ya kimkakati na hivyo kuwa na jumla ya ofisi 37 nchi nzima.
Kufikia mwezi Machi 2025, amesema ofisi hizi ndogo zimeonesha mafanikio katika kufikia wananchi walio mbali na miji mikuu ya mikoa, kuboresha udhibiti wa bodaboda, kutatua migogoro ya wadau katika maeneo hayo.

Sambamba na kufikisha elimu kwa wadau na kusogeza ushirikiano na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo hayo ikiwemo Serikali za Mitaa (LGAs), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na mamlaka zingine zilizopo kwenye maeneo hayo.
Mbali na hayo, CPA Suluo amesema,LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa hapa nchini.
Wakati huo huo, CPA Saluo amesema,LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa hapa nchini.
Pia, amesema LATRA imeanzisha njia mpya 1,007 za daladala mkoani Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi.
CPA Suluo amesema,njia za usafiri wa mabasi ya mijini zilizorefushwa kwa upande wa Dar es Salaam ni Mbezi Luis-Kisarawe kupitia barabara ya Malamba Mawili, Banana.
Nyingine ni Toangoma-Pugu Stesheni kupitia barabara ya Kilwa, Nyerere ikiwemo Kivukoni-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.
Ametaja njia nyingine kuwa ni Gerezani-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo, Buyuni Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi.
Vilevile Bunju Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale,Mbande Kisewe-Gerezani kupitia Barabara ya Kilungule, Chang'ombe, Usalama,Mvuti-Machinga Complex na Tabata Segerea.
CPA Suluo amesema, njia nyingine ni Ngobedi B-Machinga Complex kupitia Nyota Njema, na Kitonga-Gerezani kupitia barabara ya Kilwa.
Katika hatua nyingine, CPA Saluo amesema, kwa Arusha mamlaka imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na huduma.

"Mfano ni njia inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Philips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi 'Fire' na kurudi kwa Mrombo."
Akizungumzia kwa upande wa Jiji la Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi,CPA Saluo amesema,zimeanzishwa njia mpya kwa ajili yakuyafikia maeneo mapya ya makazi mapya kutokana na kukua kwa kasi kwa jiji hilo.
"Mfano wa njia hizo ni Machinga Complex-Njedengwa, Machinga Complex-Mpamaa, Machinga Complex-Chidachi, Machinga Complex-Nzuguni, Machinga Complex-Swaswa na Vyeyula-llazo."
CPA Suluo amesema,hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex imesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema,mzunguko huo ni kuanzia barabara ya Hospitali kupitia Majengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.
Katika Jiji la Mwanza,CPA Saluo amesema, zimeanzishwa njia ndefu kwa ajili ya kuyafikia maeneo mapya ya makazi na kukua kwa kasi kwa Jiji la Mwanza.
"Mfano wa njia hizo ni kutoka Usagara-Kisesa kupitia Buzuruga,llalila-Misungwi kupitia Buzuruga,Nyashishi-TX kupitia Kiseke-PPF, Nyashishi -Kisesa Kona ya Kayenze kupitia Meccov) Nyashishi -llalila kupitia Buzuruga, Mwanza mjini-lgombe, Mwaloni-Kona ya Kayenze na Mwaloni-Kabusungu."
Uthibitishaji wa Madereva
Kwa upande wa uthibitishaji wa madereva, CPA Suluo amesema, kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya LATRA Sura 413, LATRA ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafirishji vinavyodhibitiwa.
Amesema,lengo la kuthibitisha madereva ni kuwa na madereva wenye weledi wa kuendesha magari yanayotoa huduma za usafiri wa umma na mizigo kwa usalama.
“Mamlaka imekuwa ikiwasajili madereva na baadae kuwapatia vyeti vya kuthibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa inayofanyika katika Ofisi za LATRA za Mikoa yote 26 Tanzania Bara."
CPA Suluo amesema, hadi kufikia Machi 31, 2025 madereva 33,778 walikuwa wamesajiliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye Kanzidata (Database) ya mamlaka.
Kati ya madereva hao, CPA Saluo amesema, madereva 8,172 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na kupatiwa Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i-button), na madereva 4,563 walifaulu mitihani ya LATRA kati ya 9,191 waliofanya mitihani huo (sawa na ufaulu wa asilimia 49.65) na kupatiwa vyeti vya kuthibitishwa.
Matokeo haya amesema yanaashiria maandalizi hafifu kwa madereva, woga wa mitihani unaofanywa kwa kompyuta, upya wa zoezi la kuthibitisha maderevana kukosekana kwa utaratibu wa kujisomea au kujiendeleza kwa madereva.
Mabasi saa 24
CPA Suluo amesema kuwa,tangu kuanza kwa huduma za usafiri wa 24/7, LATRA imeendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani katika uratibu wa huduma za usafiri wa mabasi kwa kuimarisha usimamizi wa masharti ya leseni ikiwemo ukaguzi wa mabasi.
Pia,utambuzi wa madereva kwa i-buttons na kongeza matumizi ya VTS ambapo hadi kufikia Machi 31,2025, mabasi 2,323 yalikuwa yamepatiwa ratiba za kutoa huduma za usafiri usiku na mchana (24/7).
Aidha, tathmini ya LATRA ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa ruhusa hii ya safari za usiku na mchana (24/7) imeonesha wananchi wengi wamefurahishwa na kuridhishwa na maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mabasi kusafiri usiku.
Amesema, kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kutumia usafiri wa usiku kuliko mchana na msongamano wa abiria kwenye Stendi umepungua sana.
Pia amesema,mchezo wa mabasi kukimbizana umepungua sana na unaelekea kwisha kabisa.
Vilevile, tathmini ya LATRA inaonesha kuwa safari hizi za 24/7 zimepunguza gharama za njiani kwa abiria na kuboresha matumizi ya muda wao kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na kujiongezea vipato.
Reli
CPA Suluo akizungumzia kuhusu udhibiti wa U
Usalama wa huduma za reli amesema, usafirishaji kwa njia ya reli nchini ni mojawapo ya eneo linalodhibitiwa na LATRA kwenye maeneo ya usalama wa miundombinu na mabehewa,nauli,viwango vya ubora na ufanisi wa utendaji.
Amesema,katika hatua ya kutimiza majukumu hayo, LATRA katika kipindi kinachoanzia Februari, 2021 hadi Machi, 2025 imefanya jumla ya kaguzi 275 katika miundombinu, ishara na mawasiliano,vitembea reli (vichwa na mabehewa) na uendeshaji.
Kati ya kaguzi hizo, 143 zilikuwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), na kaguzi 132 zilikuwa kwa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Ameeleza kuwa,uanzishwaji wa huduma za Treni za SGR, LATRA ilikuwa na jukumu la kuthibitisha ubora wa vitembeareli kabla ya kuanza kutoa huduma.
"LATRA iliungana na timu ya wataalamu wa TRC na Wizara ya Uchukuzi kwenda nje ya nchi (zilikokuwa zinaundwa) na kukagua na kuthibitisha."
Amesema,jumla ya vichwa vya treni 17, mabehewa ya abiria 56, treni za seti za umeme (EMU) 10 na mabehewa ya mizigo 264 yamekaguliwa kipindi cha uundwaji katika nchi za Korea, China, Malaysia na Ujerumani.
Vilevile, mamlaka hiyo imefanya kaguzi za majaribio kwa mabehewa na vichwa hivyo baada ya kuwasili nchini kabla ya kuanza kutumika kutoa huduma.
Nauli
CPA Suluo amesema,katika mwaka wa fedha 2023/2024, LATRA ilitekeleza jukumu la kisheria chini ya Kifungu cha 5(1)(c) kwa kupanga nauli za daraja la uchumi (Economy Class) wakati wa uanzishwaji wa huduma za treni ya kisasa (SGR).
Kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya LATRA, Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA iliidhinisha nauli za abiria kwa daraja la uchumi (economy class) kwa treni inayosimama kila kituo na treni inayosimama vituo maalum (express train) na kuanza kutumika mwezi Juni, 2024.
Amesema,nauli za Treni ya SGR zilitangazwa kwa Taarifa ya Kawaida Na. 8931 kwenye Gazeti la Serikali Toleo Na 24 la 14 Juni 2024 zikiwa ni Shilingi 31,000 kwa treni ya kawaida (inayosimama kila kituo).
Sambamba na Shilingi 50,000 kwa treni inayosimama vituo maalum (express) kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Amesema,nauli zilizoidhinishwa zimeelekeza mtoto mwenye umri kuanzia miaka minne hadi miaka 12 kutozwa nusu ya nauli na mtoto mwenye umri chini ya miaka minne kutotozwa nauli.
Pia amesema, LATRA iliruhusu TRC kujipangia nauli za SGR kwa Daraja la Biashara (Business Class) na madaraja mengine ya juu (Royal Class) kwa kuwa eneo hili ni kwa abiria wenye uwezo kifedha na wanaoweza kufikia huduma hii.
Usafiri wa Waya
CPA Suluo akielezea udhibiti usafiri wa waya (Cable Transport Regulation) amesema, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa (2021/2022 hadi 2025/2026) imeelekeza maboresho katika huduma za utalii nchini.
Katika kutekeleza jukumu hili, LATRA imefanya utambuzi wa mahitaji, utayari wa wadau, na maeneo ya uwekezaji nchini.
Amesema,tathmini ya awali ya LATRA imebainisha maeneo yenye vivutio yaliyopo kwenye mikoa nane ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, na Mbeya.
CPA Suluo amesema, rasimu ya Kanuni za Udhibiti wa Usafiri wa Waya zilishaandaliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikisha wadau.
Amesema,kanuni hizo zilijadiliwa kwenye kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 23 Disemba 2024.
Pia, Bodi ya LATRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Uchukuzi, na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inakamilisha mapitio ya Muundo wa Uongozi na Mgawanyo wa Majukumu ili kuunda Kitengo cha Udhibiti Usafiri wa Waya na kuwezesha usimamizi wa Kanuni za Usafiri wa waya.
CPA Suluo amesema, zitakapokamilika zitaidhinishwa na Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 45 ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413.
TR
Naye Ofisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma,Bw. Sabato Kosuri amesema kuwa,vikao kazi hivyo vilianza Julai,2023 hadi 2024.

"Ni imani yetu kwamba mikutano 76 tuliyoifanya mwaka juzi na mwaka jana imetosha kufahamu na kupata elimu kuhusu hizo taasisi."
Amesema, kwa mwaka huu wa 2025 mwelekeo ni kupata maoni na ushauri wa namna ya kuendeleza mashirika na taasisi za umma nchini.
"Tutafanya kwa mawasilisho, tutatoa mada mbalimbali, lakini mada zitakazolenga kupata maoni, ushauri yenye kulenga kuboresha mashirika haya."
Amesema, katika awamu hii, kazi kubwa itakuwa kwa wahariri. "Sisi pamoja na mashirika tutakuwa tunachokoza mada, tunawasilisha mawasilisho, lakini tunategemea kwamba kwa sababu haya ni mashirika ya umma ni mali zetu sote, mfanye tafiti za kutosha ili mje na hoja na majadiliano yawe ni majadiliano ya kujenga."
Amesema, wameandaa utaratibu maalum wa kuyapokea maoni na hoja ambazo zitaibuliwa ili kuzifanyia kazi kwa ustawi bora wa mashirika ya umma nchini.
"Tunamini kundi hili (wahariri) ni kundi kubwa lenye maono na uwezo mkubwa wa kuweza kusaidia Serikali yetu."
Msemaji Mkuu wa Serikali
Kwa upande wake Mwakilishi wa Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Revocatus Kassimba ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Shirika la Masoko Kariakoo amesema kuwa, Msemaji Mkuu wa Serikali anaipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Ni kwa kuendeleza utamaduni huu ambao unawakutanisha wahariri pamoja na wanahabari mbalimbali nchini.
Lengo likiwa ni taasisi na mashirika ya umma kuelezea kwa kina mafanikio mbalimbali ambayo yamepatikana katika kipindi chote cha utekelezaji wa shughuli zao.
"Msemaji Mkuu wa Serikali anawapongeza sana Ofisi ya Msajili, anaomba muendelee na utaratibu huo."
Jambo lingine, amesma Idara ya Habari Maelezo itaendeleza ushirikiano na wahariri pamoja na waandishi wa habari kote nchini.
"Itakumbukwa kuwa, Msemaji anasema huo utaratibu wa kukutana na vyombo vya habari unaendelea, wanaofanya kazi hizi kwa kiwango kikubwa kule mikoa ni waandishi wa habari ambao wanatoka kwenye taasisi zenu."
Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali amewahimiza wahariri na wanahabari kutoa elimu ya kutosha hususani kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba.
"Kwa hiyo, pia tunalo jukumu kubwa la kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kwanza kupiga kura."
Pia, amesema jambo kubwa ambalo wanategemea vyombo vya habari vifanye ni kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa misingi ya haki.
"Tudumishe amani kupitia kazi za kalamu zetu tunazozitumia, vyombo vya habari viwe taasisi ya kuhamasisha amani na usalama wakati wote wa uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi mkuu."

"Waandishi wa habari mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha umma unatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Serikali."
Tags
Breaking News
Habari
Kikao Kazi Msajili wa Hazina
LATRA Tanzania
Makala
Ofisi ya Msajili wa Hazina