MANYONI-Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kubadili maisha ya Wakazi wa Mji wa Manyoni, Singida kwa uwekezaji mkubwa wa mradi wa maji wa miji 28.

Mradi huo unalenga kuwanufaisha zaidi ya wakazi elfu sitini na nne wa mji wa Manyoni, na kuleta mapinduzi kwa kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo kuwa asilimia 100 kutoka asilimia 78 ya sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manyoni (MAUWASSA), Mhandisi Lucas Mwinuka, amesema kuwa ujenzi wa mradi umefika asilimia 45.
"Tumekamilisha uchimbaji wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha jumla ya lita 270,000 kwa saa na ujenzi wa tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 pia umekamilika," Mhandisi Mwinuka ameainisha.
Kazi nyingine zilizokamilika ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu la maji lenye urefu wa kilomita 14.1 kutoka kituo cha visima, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji ukiwa umefika asilimia 70.
Kazi ya ulazaji wa mabomba ya usambazaji ya maji yenye urefu wa kilomita 30 inatarajiwa kuanza Juni 2025 baada ya usanifu kukamilika.
Diwani wa Kata ya Manyoni, Mhe. Samuel Lupembe, amepongeza jitihada hizo na kusema kuwa wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakisubiri mradi huo kwa muda mrefu kutokana na upungufu wa huduma ya maji na ongezeko la wananchi.

Naye, Fatuma Shabani, mkazi wa Kitongoji cha Chang’ombe, amesema mradi huo si tu unawaletea faraja ya kupata maji ya nyumbani, bali pia unafungua fursa mpya za kiuchumi kwa kina mama na vijana kupitia shughuli zitakazotegemea maji.
"Kwa mara ya kwanza, tunaona tumaini jipya kwa maendeleo ya wanawake. Tunaweza kufikiria kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi kama bustani, ufugaji wa kuku, na shughuli nyingine zitazoimarisha kipato chetu," Fatuma ametoa shukran kwa Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuwaona kina mama na mahitaji yao.

Mradi huo ni ushahidi wa utekelezaji wa Serikali ikuwekeza katika huduma za msingi kwa wananchi kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jamii, kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuijenga Tanzania yenye majisafi kwa wote.