DAR-Muhibiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba (Fireman) ametoa onyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku akisema kipindi kile cha kampeni hakikuwa sahihi kwa Tundu Lissu,amesisitiza kuna anguko kubwa linakuja katika chama hicho.
Amesema, Lissu alipaswa kuwa Mwenyekiti kuanzia mwaka 2030, kwani kwa nyakati hizi, Mbowe alipaswa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
"Mbowe angekuwa kiongozi wa CHADEMA uchaguzi huu,ingepata wingi wa wabunge na ingeweza kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi kama chama kikuu cha upinzani."
Temba ameeleza kuwa,tayari wapiga kura walio wengi ikiwemo wa CCM walishaona chama hicho hakina tatizo, kwani chuki ya awali iliondolewa kwa njia ya maridhiano.
Amesema, maridhiano hayo ndiyo yalifanikisha pia Tundu Lissu kurejea nchini ikiwa na yaliongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya Mbowe na heshima aliyoijenga kwa muda mrefu, Temba amesema hakukutakiwa kuwa na kampeni za kumdhalilisha.
Amesema, licha ya Mbowe kushindwa kwa ushindi mwembamba huku akidhalilishwa yeye na familia yake, bado ndani ya chama kuna watu wengi wanamkubali na kumheshimu.
"Kitendo cha Mheshimiwa Tundu Lissu mara tu baada ya kupata uenyekiti akaanzisha misimamo ambayo ni kinyume na jina lililoko katika chama hicho la Demokrasia na Maendeleo kwamba maamuzi yake yeye na makamu wake Heche hayapingwi na Mjumbe wa Kamati Kuu, Lema hayapingwi na ni misimamo ambayo inasimamiwa na Maria Sarungi kwa muda mrefu, haina afya kwa ustawi wa chama."
Temba amesema, kwa muda mrefu watu wengi wanaona ndani ya chama hicho kuwa, Lissu anatumika tu kama bendera.
Lakini, amesema mwenye nguvu ya kusimama na kusema ikiwemo kuhoji ni Maria Sarungi na genge lake ikiwemo Diaspora wengi waliopo nje ya nchi.
"Ambao waliahidi kutuma fedha nyingi kupitia Dkt.Willbroad Slaa kipindi cha kampeni na fedha nyingi zilienda mikoani kwa ajili ya kumchafua Mbowe."
Kwa muktadha huo,Temba amesema ndiyo maana kipindi cha kampeni vijana wengi waliibuka mikoani wakishinikiza Lissu achaguliwe, kwani viongozi wao wakirudi bila ushindi wa Lissu hawatawaelewa.
"Kulikuwa na vitisho vingi sana visivyo vya kawaida, kulikuwa na nguvu kubwa sana ambayo CHADEMA haijawahi kutumia hata wakati wanagombania na vyama vingine vya upinzani kwa ajili ya kupata nafasi za uongozi."
Mbali na hayo, ametoa ushauri kwa Serikali kuangalia namna ya kudhibiti kauli zenye viashiria vya kuchochea machafuko nchini, kwani mara nyingi kinywa Lissu na wenzake vimekuwa vikitoa maneno ya uchochezi ambayo ni hatari kwa ukuaji wa uchumi.
Temba amesema, kwa mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hatuwezi kuiweka nchi katika hali ya hofu.
"Mfano unahamasisha watu kugoma, kuandamana na kuandamana hawatangazi wanaandamana kwenda wapi, kwenda kufanya nini? Na mwisho wa maandamano itakuwaje, yatakwenda kwa muda gani."
Amesema, hali hiyo inaweza kuwapa shaka wawekezaji hususani wenye viwanda vingi mkoani Pwani.
"Hofu kubwa zikijengwa wengine watafikiri kwamba maandamano hayo yanaweza kwenda kuchoma viwanda vyao, kwenda kuwazuia wafanyakazi wao na kadhalika hivyo ikapunguza morali ya wawekezaji hawa kufungua kazi kubwa, kuleta mitaji mingi katika taifa na kazi yote iliyofanyika katika awamu hii ya Sita ikawa ni kazi bure.
"Hivyo, Tundu Lissu anapaswa akae kwenye maneno yake mwenyewe, alivyokuwa Nairobi akijitetea kwenye vyombo vya nje vya Kimataifa kwamba atakwenda kugombea urais na Mwenyekiti Mbowe hata akigombea na mwingine akitangaza kugombea ubunge na udiwani na si kosa kwa sababu maamuzi yatafanyika.
"Kwa nini hawaruhusu maamuzi kufanyika, matokeo yake tunaona kule Iringa kwamba kiongozi wa CHADEMA mwana mama yule alipigwa kwenye vikao na inatumika nguvu kubwa tena, vikao hivyo hivyo vilivyompiga kuchunguza na kumtishia kwamba endapo atagundua tofauti watamchukulia hatua, kitu ambacho kinaendelea kuwashangaza watu wengi."
Katika uongozi wa Freeman Mbowe, Mwinjilisti Temba amesema, licha ya masingizio kadhaa hakujawahi kufanyika vituko kwa muda mfupi.
"Au kwa muda mrefu aliokaa madarakani, kama hivi tunavyovishuhudia sasa, kutokuelewana katika chama na kadhalika, Tundu Lissu anapaswa kujua kwamba lazima arudi kumuomba radhi Mbowe."
Amesema, ni kwa sababu alipata uongozi huo kwa kumkashifu, kumtukana kibabe na kumdharau ndiyo maana mambo yamekuwa hovyo.
"Haya anayoyapata Tundu Lissu, ni Mungu anarudisha kwake kwa sababu hakuwa chaguo la Mungu, hivyo ni vema Watanzania wakajua mapigo yanayopatikana CHADEMA ni mkono wa Mungu na sio kukimbilia kuwatukana watu wale ambao wanakataa kunyanyaswa.
"Haiwezekani kwamba, uchaguzi wa kushinda Heche na Lissu ndiyo useme au isemekane kuna Demokrasia, lakini wanachama wengine ambao wanataka na wao ama washinde ama wagombee ama watoe fikra zao kwenye ndani ya vikao na nje ya vikao waonekane waasi, wanatumika na system,
"Wanatumika na Chama Cha Mapinduzi na wanatumia hii kwa sababu Lissu amejikuta hana hoja, anaendeshwa na Watanzania walioko nje na sasa hivi tumeona dhairi walikuwa wakitangaza Tone Tone kila kiasi cha fedha kilichopatikana, mara ya mwisho walisema milioni 20, wakasema milioni 50, lakini kwa sasa wamekaa kimya mpaka sasa haijulikani kiasi gani kimepatikana na hazitangazwi.
"Na Lema ambaye alikuwa akifanya mikutano, mjumbe wa kamati kuu kwa ajili ya kusimamia hilo na kutoa taarifa naye amekuwa kimya, matokeo yake ndiyo anapambana watu wasigombee ubunge, wala urais kwenye chama cha CHADEMA kwa sababu wanajua hawana fedha.
"Hata ya kufanya mikutano mitano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wameamua kuifia No Reform No Election kuficha aibu yao."
Temba amesema, Watanzania wanaendelea kusubiri na kuangalia mwisho utakuwaje.
"Mheshimiwa Mbowe chagua kunyamaza ni mpango wa Mungu,soma Kutoka 14.14 Bwana atawapigania nanyi mtanyamaza kimya."
KWA HOJA AU SWALI
Email:phonce2003@yahoo.com
Simu:0747646299