DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kuendelea kudumisha amani ya nchi na kubaki kwenye jukumu la kuwalea wananchi kiroho.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo katika Baraza la Eid El-Fitr lililofanyika kitaifa Mkoa wa Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha,Rais Dkt.Samia amewasisitiza viongozi wa dini zote nchini kutoruhusu majukwaa ya kiimani kutumika kuhubiri siasa, au ajenda za kisiasa kuvuruga amani ya nchi kupitia majukwaa ya ibada.
“Muwadhibiti wachache walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki dhidi ya Serikali yao. Ni vyema tujue katika mifarakano na hasama hakuna atakeyeibuka mshindi.

"Jukumu la kusimamia amani ni la Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama lakinipia ni jukumu la wananchi wote," amesema Rais Dkt. Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameweka wazi kuwa kamwe Serikali haitamvumilia yeyote atakayechochea chuki na uhasama na kusababisha uvunjifu wa amani, bali Serikali imejidhatiti kulinda haki na utu wa kila Mtanzania.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amewasihi waislamu kuwa wanaposherehekea EidEl-Fitr waendeleze ucha Mungu waliouonesha katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kuzilinda ibada zao na kudumisha umoja na mshikamano waliokuwa nao kipindi cha mfungo.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Samia amewasisitiza wadau wote wa kisiasa kutimiza wajibu wao na kutokuruhusu itikadi za kisiasa kuwagawa Watanzania.
Halikadhalika, ameeleza kuwa milango ya Serikali iko wazi kusikiliza madai ya wadau wakisiasa kupitia majukwaa mbalimbali ambayo yanawapa nafasi ya kuzungumza namajukwaa ambayo yaliwezesha mageuzi mbalimbali kufanyika kwa kuwashirikisha wadau wote wa kisiasa, ikiwemo kufutwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa nakuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.