Rais Dkt.Samia mbioni kuandika historia nyingine ya reli Dar

NA GODFREY

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ipo mbioni kuanza ujenzi wa reli ya Jiji la Dar es Salaam (Commuter Rail Network).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, akitoa wasilisho wakati wa kikao kazi cha pamoja baina ya Menejimenti ya TRC na Wanahabari wa mitandao ya jamii, kinachofanyika mkoani Morogoro. Kikao kazi hicho kinalenga kutoa elimu, maarifa na stadi za namna bora ya kuripoti habari za Reli.

CRN ni mtandao wa reli unaohusisha usafiri wa treni zinazotumika kubeba abiria kwa umbali mfupi hadi wa kati, hasa katikati ya miji na maeneo yake ya pembezoni.

Utekelezaji wa mradi huo,utahusisha treni zinazofanya safari kwa njia za umma ambapo abiria watakuwa wakitumia treni kusafiri kwenda na kurudi kutoka kazini, biashara, vituo vya afya, shuleni, nyumba za ibada na kwingineko.

Kadogosa amesema, utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji huduma bora za usafirishaji kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo ya jamii na Taifa.

"Kwa hiyo, reli ya Dar es Salaam ni must,"amesema Kadogosa huku akibainisha kuwa, uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na Taifa.

Mkurugenzi Mkuu huyo ameyasema hayo leo Aprili 3, 2025 mkoani Morogoro katika kikao kazi kati ya uongozi wa TRC na wanahabari mbalimbali wa mitandao ya kijamii.

Amesema, utekelezaji wa treni za namna hiyo utaenda jijini Dodoma na huko utaanza mapema zaidi, na baadaye utaelekea Arusha na Mbeya.

"Usanifu wa awali na upembuzi yakinifu umekamilika kwa upande wa ujenzi wa Reli ya Jiji la Dar es Salaam, pia Dodoma umekamilika, na tutaanza mapema zaidi, kwa sasa hatua za utafutaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli zinaendelea."

Kadogosa amesema, miradi hiyo inatarajiwa kufanyika kwa kushirikisha sekta binafsi (PPP) ambapo kampuni mbalimbali zimejitokeza. "Na zimeonesha nia ya kushiriki katika ujenzi wa njia hizo ikiwemo Kampuni ya Alstom."

Jitihada hizo zinaenda sambamba na utekelezaji wa majikumu ya shirika hilo kutokana na lengo kuu la kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo kusimamia na kuendeleza miundombinu ya reli.

Kuhusu uendelezaji wa miundombinu mipya ya reli, Kadogosa amesema kuwa, jukumu hilo linajumuisha usanifu na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.

"Jukumu lingine, TRC inatoa huduma za usafiri kwa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi, hii inajumuisha huduma za ukodishaji."

Vilevile amebainisha kuwa, shirika hilo la umma chini ya Wizara ya Uchukuzi linawajibika kuimarisha na kuongeza vitendea kazi vya injini, mabehewa na mitambo ya mawasiliano.

Wakati huo huo, Kadogosa ameendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hasasn kwa kuwekeza nguvu nyingi katika utekelezaji wa miradi ya SGR ambayo imeonesha matokeo chanya nchini.

"Kwa sasa utekelezaji wa mradi wa SGR unaendelea katika awamu mbili na jumla ya thamani ya mikataba iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa SGR ni takribani shilingi trilioni 29.580."

Aidha, kutokana na kazi kubwa inayofanywa na shirika hilo,Burundi imeiamini Tanzania kupitia TRC ili kuwapa mafunzo wataalamu wao kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli kutoka Uvinza kwenda Musongati nchini Burundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news