Serikali yatakiwa kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu

ZANZIBAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dkt.Haroun Ali Suleiman amesema,Tanzania kama nchi inayohusika na mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu pamoja na itifaki ya haki za wanawake Afrika inapaswa kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wake kwa wakati.
Ameyasema hayo wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha kupitia Rasimu ya Taarifa ya Nchi ya utekelezaji wa mikataba hiyo kilichofanyika Hoteli ya Madinatul Al bahr Mbweni Zanzibar.

Dkt.Haroun alisisitiza kuwa, kuna umuhimu wa nchi kutoa taarifa ya utekelezaji wa mikataba hiyo kwani kunajenga uwazi, uwajibikaji, na imani ya kimataifa kuhusu juhudi za Tanzania kulinda haki za binadamu.

Aliongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia katika kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kusaidia wahanga wa ukiukwaji wa haki, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

"Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi iliyorodhia mikataba hiyo tuna wajibu wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji katika kila kipindi husika,"alisema Dkt.Haroun.

Aidha, Dkt.Haroun aliwahimiza washiriki wa kikao hicho kujitahidi kutoa maoni yenye tija ili kuandaa taarifa inayoonyesha dhamira ya nchi katika kulinda haki za binadamu.

Alisema, endapo watashiriki vyema wataisaidia nchi yao kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Katika mkataba na itifaki ya Maputo ilioandaliwa vizuri na kuleta manufaa Kwa Taifa.

Alibainsiha kuwa, kuandaa taarifa yenye kukidhi viwango kutaleta taswira nzuri hasa matika jumuiya za kimataifa kwani itaonyesha dhamira ya nchi Katika kulinda na kutetea haki za binaadamu zikiwemo za makundi maalum.

Alisema pamoja na kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imeridhia mikataba hiyo,lakini pia ni nchi inayolinda na kutetea haki za binaadamu kwa vitendo.

"Serikali imechukua hatua Mbali Mbali Katika kulinda, kuhifadhi, na kukuza haki za binaadamu kama zilivyoanzishwa Katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 ambapo imetaja haki za binaadamu kuanzia ibara ya 12-24 na katiba ya zanzibar imeanzisha haki hizo kuanzia kufungu cha 11-25A,"alieleza Dkt.Haroun.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa taarifa ya haki za binaadamu kutoka Wizara ya katiba na sheria Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Beatrice Mpembo alisema,lengo la kikao hicho ni kupitia na kujadili rasimu ya taarifa za nchi juu ya utekelezaji wa mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu na itifaki ya haki za wanawake Afrika.

Hivyo ushirikiano wa wadau hao utatusaidia kubaini hatua za utekelezaji wa mikataaba hiyo, pamoja na changamoto za utekelezaji na kuja na njia bora za kuboresha utekelezaji wa mikataba huo.

Mapema alibainisha kuwa kikao hicho ni muhimu kwani kitatoa fursa ya kupitia na kujadili hatua zilizochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa mkataba huo.

“Utekelezaji wa mikataba huu, ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda na kukuza haki za binadamu na haki za wanawake hapa nchini.”

Aidha, alisema mikataba hiyo inatoa miongozo kwa nchi wanachama kuhakikisha sheria, sera na mikakati inalenga katika kulinda na kutetea haki za binadamu.

Pamoja na hayo, alileza kuwa kikao kitazingatia maeneo muhimu kama vile haki za wanawake, usawa wa kijinsia, haki za watoto na haki za makundi maalum,na namna nchi inavyoshirikiana na jumuiya za kimataifa katika kuhakikisha kuwa haki hizo zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa kiwango kinachohitajika.

“Kupitia kikao hichi, washiriki watapata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo, ambayo yatasaidia kuishauri Serikali juu ya namna bora ya kutekeleza mikataba hii, ili kufikia malengo ya kulinda haki za binadamu nchini,"alisema.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho walisifu juhudi za wadau hao na kusema kuwa kushiriki kwao kumewapa fursa ya kutoa maoni, kukosoa na kuichangai taarifa hiyo kwa lengo la kuiboresha.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Salma Haji Saadati alisema, kutokana na kuwa mkataba huo unazungumzia masuala mengi ikiwemo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa hivyo wangependa kuona hatua za utekelezaji katika taarifa hiyo.

Alieleza kuwa, kuna umuhimu wa kuendelea kusimamia na kutekeleza mkataba huo ili kufikia usawa wa kijinsia unaowalinda wanawake dhidi ya ubaguzi vurugu na vitendo vya ukatili.

Kikao hicho kilichowashirikisha wadau wa asasi za kiraia, kililenga kupitia hatua zilizochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa mikataba hiyo, na pia kutathmini ushirikiano na jumuiya za kimataifa ili kuhakikisha kwamba haki za binadamu zinatekelezwa kwa kiwango kinachohitajika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news